Katika mkutano huo uliofanyika mjini Paris, washirika hao wameongeza kuwa wako tayari kutoa dhamana za kimataifa ili kuzuia Moscow kushambulia tena Ukraine.

Dhamana hizo zinatarajiwa kujumuisha msaada wa kijeshi, ufuatiliaji wa kimataifa na hatua za kuzuia ukiukaji wa makubaliano yoyote ya amani.

Mojawapo ya mapendekezo yaliyowasilishwa ni pendekezo la Marekani kuongoza juhudi za kufuatilia utekelezaji wa usitishaji mapigano. Hatua hiyo ingeipa Washington jukumu la moja kwa moja katika kudumisha amani yoyote itakayofikiwa kati ya Ukraine na Urusi.

Mkutano huo ulihudhuriwa na viongozi kutoka nchi 27 za Ulaya, pamoja na Canada, wawakilishi wa Marekani, maafisa wakuu wa Umoja wa Ulaya, na viongozi wa jumuiya ya kujihami ya NATO.

Huu ulikuwa mkutano wa 15 wa kile kinachoitwa “muungano wa walio tayari kuisaidia Ukraine”, lakini pia ndio mkutano mkubwa zaidi kuwahi kufanyika tangu muungano huo uanzishwe.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *