Jamii ya wamasai iko katika hatari kubwa TanzaniaJamii ya wamasai iko katika hatari kubwa Tanzania

Mzozo kuhusu matumizi ya ardhi unaendelea kukua na hali ya watu kufukuzwa kutoka kwenye ardhi ya mababu zao ili kuendeleza miradi ya utalii, tayari imezisukuma ukingoni baadhi ya jamii za Wamaasai katika maeneo hayo.

Eneo la Mlima wa Mungu, ambalo kwa lugha ya Kimaasai wanaliita Ol’doinyo Lengai ni eneo lililoko kilomita chache kutoka mji wa Engare Sero kaskazini mwa Tanzania. Na pembeni ya mji huo ndiko lilipo Ziwa Natron, ziwa la chumvi linalong’aa na kupendeza.

Linachukuliwa kuwa eneo muhimu zaidi kutokana na kwamba asilimia 75 ya Flamingo adimu ambao idadi yao ni ndogo sana duniani wanalitumia kwa kuzaliana. Flamingo hao ni tofauti kabisa na Flamingo wengine, wana rangi ya waridi inayong’aa, miguu mirefu, na midomo yao ina ncha nyeusi.

Lakini pia ni eneo muhimu kwa jamii wa Wamasai, ambao nao wanaichukulia sehemu hiyo kuwa ni ardhi yao waliyorithi kutoka kwa mababu zao na wengi wao wanahofia juu ya hatua zinazokuja za kuwafukuza kwa wingi kutoka kwenye eneo lao.

Tanzania Ngorongoro 2025 | Wamasai wa Ngorongoro
Mzozo kuhusu matumizi ya ardhi unaendelea kukua na kusukuma ukingoni jamii za Wamaasai.Picha: Marco Simoncelli/DW

Mmoja wao ni Nesikar Daudi mwenye umri wa miaka 36, ambaye ameeleza kuwa alilazimika kukimbia nyumbani kwake baada ya sehemu hiyo kugeuzwa kuwa hifadhi ya uwindaji ya Pololeti.

Mnamo mwaka 2022, serikali ya Tanzania ilianzisha Hifadhi ya Wanyama ya Pololeti, na kuiteua kwa ajili ya uwindaji na utalii pekee. Maelfu ya watu, kama Nesikar, waliathiriwa moja kwa moja huku wengine hata wakifukuzwa kwa nguvu.

“Tuliteseka sana kutokana na uporaji huu wa ardhi. Tulipoteza mifugo yetu, na matingatinga yalibomoa nyumba zetu,” alisema mama huyo.

Tangu miaka ya 90, Tanzania imepanua maeneo yaliyohifadhiwa kwa asilimia 20. Lakini wakili na mwanaharakati wa Kimaasai Joseph Oleshengay amesema mkakati wa serikali katika miaka ya hivi karibuni hauna uhusiano wowote na uhifadhi wa asili bali kimsingi ni utaratibu wa kuwanyang’anya Wamaasai ardhi yao kwa kisingizio cha ulinzi wa mazingira. Wakili huyo ameiambia DW kwamba kuna maslahi ya kiuchumi yanayohusiana na utalii na uwindaji wa nyara. Amesema nia hasa ni kuwaondoa watu kabisa kutoka kwenye maeneo haya ili yaweze kugeuzwa kuwa mradi unaoingiza pesa.

Tanzania Napandi | Masaibu ya jamii ya wamasai Tanzania
Karibu asilimia 43 ya eneo la Tanzania sasa linaangukia katika aina fulani ya eneo linalolindwa.Picha: Marco Simoncelli/DW

Wakili na mwanaharakati wa Kimaasai Joseph Oleshengay amesema mamlaka hufanya kazi chini ya sheria inayoruhusu ardhi yote nchini Tanzania kuainishwa upya ikiwa itaonekana kutumikia “maslahi ya umma.” Kiuhalisia, mkuu wa nchi anaweza kuamua hatima ya maeneo yote bila wajibu wowote wa kushauriana na jamii zinazoishi humo.

Wamasai wametengwa katika miradi ya utalii

Tanzania ina maeneo ya wanamapori yanayodhibitiwa yaani Game-Controlled Areas (GCA) na maeneo ya usimamizi wa wanyamapori- Wildlife Management Areas (WMA). Yote yamefafanuliwa rasmi kama zana za kulinda wanyamapori na mazingira, lakini hutofautiana katika sheria zake na jinsi zinavyoathiri jamii za wenyeji.

Katika GCA na WMA, shughuli za binadamu zimezuiliwa lakini hazijatengwa kabisa. Maeneo ya WMA huruhusu makazi, ufugaji, na wakati mwingine kilimo lakini katika maeneo yaliyo chini ya sheria ya GCA, kilimo ni marufuku, na malisho ya Wanyama yanaruhusiwa tu kwa kibali maalum kutoka kwa mamlaka husika, huku makazi yakibaki kuwa yanaruhusiwa. Hata hivyo, katika hifadhi za wanyamapori kama Pololeti, uwepo wa binadamu umepigwa marufuku kabisa.

Kuondolewa kwa Wamasai Tanzania ni maendeleo au dhulma?

To view this video please enable JavaScript, and consider upgrading to a web browser that supports HTML5 video

Karibu asilimia 43 ya eneo la Tanzania sasa linaangukia katika aina fulani ya eneo linalolindwa. Kwa pamoja, hifadhi za wanyamapori, zilizo chini ya sheria za GCA na WMA zina ukubwa wa takriban kilomita za mraba 159,000,ambalo ni eneo kubwa kuliko taifa jirani la Malawi.

Ripoti ya ndani ya Wizara ya Maliasili na Utalii, kulingana na mpango wake wa kimkakati wa 2021–2026, inaonyesha kwamba maeneo 15 mapya karibu kilomita za mraba 7,000  yamepangwa kubadilishwa kutoka maeneo ya wanyamapoti yanayodhibitiwa GCA na kugeuzea na kuwa hifadhi za wanyama. Mradi huo, ambao utaathiri maisha ya maelfu ya ya watu, pia mradi huo unajumuisha kilomita za mraba 4,000 katika eneo la Ziwa Natron.

Dola za watalii zavutia

Kwa miaka mingi, serikali ya Tanzania imejaribu kuwafukuza wakazi kutoka kwenye eneo hilo la mababu zao kwa sababu, inalitazama eneo hilo kuwa ni la kimkakati kwa shughuli za utalii.

Ardhi inayozunguka ziwa Natron takriban kilomita za mraba 3,000 tayari limeainishwa kama eneo la wanyamapoti linalodhibitiwa, GCA, huku vitalu vinne vya uwindaji vikikodishwa kwa makampuni binafsi ambayo hulipa ada ya kila mwaka ya hadi dola 300,000 kila kimoja.

Tansania | DW-Reportage
Wamaasai, ambao hapo awali walitembea kwa uhuru wakitafuta malisho, mipaka na vikwazo hivi vipya vimepunguza kwa kiasi kikubwa ardhi ya kuweza kulisha mifugo yao.Picha: Marco Simoncelli/DW

Wateja ni watu kadhaa mashuhuri. Mnamo tarehe 8 Juni 2023, Donald Trump Jr. mwana wa rais wa Marekani, aliitembelea Tanzania, ikiwa ni pamoja na eneo la Ziwa Natron. Kulingana na vyombo vya habari vya ndani na vyanzo vilivyo karibu na TAWA (Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania), alitumia maelfu ya dola kwenye safari iliyojumuisha uwindaji mkubwa.

Huduma za vijijini zimepunguzwa

Mamlaka pia zimelenga huduma muhimu za afya, katika eneo hilo la ziwa Natron zikiakirudia mifumo inayoonekana katika maeneo mengine kama vile Ngorongoro.

Maeneo kama Ziwa Natron, Pololeti, na mengine yaliyotengwa kwa ajili ya hifadhi za wanyamapori yako kando ya njia muhimu za uhamiaji wa wanyamapori: karibu na mbuga kubwa za kitaifa, na karibu na mpaka wa Kenya. Ingawa mradi huu ni thamani kubwa kwa uhifadhi na utalii, lakini jamii za wafugaji ziko hatarini.

Kwa Wamaasai, ambao hapo awali walitembea kwa uhuru kati ya Tanzania na Kenya wakitafuta malisho, mipaka na vikwazo hivi vipya vimepunguza kwa kiasi kikubwa ardhi ya kuweza kulisha mifugo yao.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *