Bila shaka zaidi ya asilimia sabini ya vijana hawamjui rais mwengine tangu walipozaliwa ila yeye ambaye ametawala kwa miaka 40. Vijana wana mitazamo tofauti kuhusu uongozi wake. Huku wengine wakielezea kuwa wanapendelea aendelee kutawala kutokana na mazingira ya amani na uthabiti ambayo amedumisha, wengine wanapinga kabisa. Wanadai kuwa utawala wake ndicho chanzo cha hali ngumu ya maisha ambayo imewakosesha kutimiza ndoto zao.
Kutokana na idadi kubwa ya vijana kuonyesha kutoridhirishwa na utawala wa rais Museveni, wanamuunga mkono Robert Kyagulanyi maarufu kama Bobi Wine. Kwa mtazamo wao, yeye anayefahamu zaidi changamoto na fursa za kizazi hiki hasa kutokana na safari yake ya maisha kutoka mitaa ya mabanda maarufu kama Ghetto hadi kufikia ngazi ya utajiri na umaarufu.
Aidha wanamwona kuwa mtu ambaye uzalendo wake unalenga kuondoa kabisa ubaguzi wa kikabila, kidini, kitabaka na kupambana na rushwa pamoja na kurejesha utawala wa kikatiba na kisheria ambavyo wengi wanasema ndiyo mambo ambayo yamedoroza demokrasia na haki za binadamu Uganda. Mchambuzi wa masuala ya kisiasa Monday Akol Amazima anatoa angalizo hili:
“Siasa za Bobi WIne zimekuwa za kutoa mwamko mpya hasa kwa vijana.”
Museveni aanzisha miradi ya kutoa fedha na mitaji kwa vijana
Rais Yoweri Museveni anafahamu kuwa vijana ambao yeye huwaita wajukuu zake wana ushawishi mkubwa katika siasa mamboleo. Ametumia vichocheo na hila mbalimbali kuwashawishi na hata kutumia matamshi ambayo baadhi wanasema ni ya vitisho dhidi yao. Kamatakamata na hujuma dhidi ya vijana wa upinzani ni hali ambayo imeshuhudiwa tangu mwaka 2020 na wengi wangali magerezani hadi sasa.
Kwa upande mwingine ameanzisha miradi mbalimbali ya kutoa fedha na mitaji kwa vijana akilenga hasa wale wa kizazi kinachojulikana kama wazawa wa Ghetto kama namna ya kuitikia vilio vyao vya ukosefu wa kazi. Lakini si rahisi kuwashughulikia vijana wote changamoto zao na ndiyo maana baadhi wanasema afadhali akabidhi madaraka kwa mtu mwingine wa kizazi chao kwa njia ya amani.
Kwa mujibu wa hilo, rais Museveni ameonekana kumwandaa zaidi mwanawe Jenerali Muhoozi Kainerugaba ambaye kwa sasa ni mkuu wa majeshi. Mchambuzi Akol Amazima ana kauli hii kuhusu mchakato wa kumrithi Museveni:
“Angekuwa ameshawandaa watu labda wengine wangemwambia “umeshamwandaa fulani, mpishi” lakini kwa sababu walehawajajiandaa vya kutosha labda ndiyo sababu amekuwa akijiongezea muda na wengine wanamwongezea.”
Kutokana na udhibiti wake kwa taasisi za utawala na sheria na kuwa na uwezo wa kufadhili kampeni zake, wengi wanaamini rais Museveni atatangazwa mshindi katika uchaguzi utakaofanyika wiki ijayo tarehe 15. Mojawapo ya njia za vijana wa upinzani kushawishi maamuzi ya wapigaji kura pamoja na matokeo ya uchaguzi ni kuzidi kumnadi mgombea wao Bobi Wine kupitia mitandao ya kijamii. Hata hivyo kama ilivyokuwa katika uchaguzi uliopita, kuna mashaka kama mitandao haitazimwa. Mamlaka ya mawasiliano UCC imesema kuwa safari hii haitafanya hivyo.
