Muungano wa kijeshi unaoongozwa na Saudi Arabia umesema siku ya Alhamisi kwamba Aidaros Alzubaidi yuko katika Umoja wa Falme za Kiarabu, baada ya jaribio lake la kukamata maeneo makubwa na kutaka uhuru wa maeneo hayo. 

Duru za kuaminika za kiintelijesia zimeashiria kwamba Aidaros Alzubaidi na washirika wake wengine walitoroka usiku wa manane kutoka Yemen. Hayo ni kulingana na taarifa kutoka Muungano wa kijeshi unaoongozwa na Saudi Arabia.

Taarifa hiyo imeanisha safari ya al-Zubaidi kutumia boti kutoka mji wa Aden hadi Berbera jimbo la Somaliland, kisha akaabiri ndege hadi Mogadishu Somalia chini ya ulinzi wa maafisa wa Umoja wa Falme za Kiarabu UAE, safari iliyomfikisha katika uwanja wa ndege wa kijeshi mjini Abu Dhabi.

Hata hivyo hakukuwa na taarifa ya moja kwa moja kutoka katika wizara ya Mambo ya Nje ya Umoja wa Falme za Kiarabu kuhusu madai hayo.

Aidaros Alzubaidi, ambaye ni kiongozi wa Kundi la waasi lijulikanalo kama Southern Transitional Council (STC) yaani Baraza la Mpito la Kusini, ambalo linaungwa mkono na UAE, alituhumiwa kwa makosa makubwa ya uhaini na hivyo kutimuliwa kutoka kwenye Baraza la Uongozi wa rais nchini Yemen siku ya Jumatano.

Mpasuko kati ya Saudi Arabia na UAE kuhusu Yemen

Hayo yalijiri wakati vikosi vya muungano unaoongozwa na Saudi Arabia vikishambulia mkoa wake wa nyumbani al-Dhale, vikimtuhumu kuandaa vikosi vikubwa vya kijeshi, hasa baada ya kukataa kuhudhuria mkutano ulioandaliwa Riyadh kwa mazungumzo.

Yemen Aden 2026 | Maandamano ya wanaotaka uhuru wa majimbo ya Kusini mwa Yemen
Wafuasi wa waasi wa STC nchini Yemen wanaounga wito wa uhuru wa Majimbo ya kuisini mwa nchi hiyo.Picha: AP Photo/picture alliance

Mwezi uliopita, mashambulizi ya STC yalisababisha msukosuko mpya nchini Yemen, taifa maskini zaidi na lililogawika katika Rasi ya Kiarabu. Mashambulizi hayo pia yalifichua mpasuko mkubwa kati ya washirika wa Ghuba, Saudi Arabia na UAE.

Majirani hao wa Yemen wenye utajiri mkubwa wa mafuta ndio waliounda uti wa mgongo wa muungano wa kijeshi unaopambana na waasi wa Wahouthi wanaoungwa mkono na Iran nchini Yemen, ambao waliteka mji mkuu Sanaa mwaka 2014 na bado wanadhibiti sehemu kubwa ya nchi.

Riyadh na Abu Dhabi sasa wamejikuta wakiiunga mkono kambi zinazoshindana ndani ya serikali ya Yemen ikiwemo STC.

Saudia yazima jaribio la STC Hadramawt na Mahra

Mwezi Disemba, waasi wa STC walielekea katika majimbo ya Hadramawt na Mahra yanayopakana na Saudi Arabia na Oman, lakini walilazimika kurudi nyuma baada ya Saudi Arabia kutumia ndege zake za kivita kuwashambulia huku vikosi vinavyounga mkono Saudi Arabia pia vikiwashambulia ardhini.

Awali muungano unaoongozwa na Saudi Arabia ulimpa al-Zubaidi muda wa saa 48 afike Riyadh kwa mazungumzo. Hata hivyo, al-Zubaidi hakupanda ndege iliyokuwa imeubeba ujumbe wake.

Wakati ndege za kivita za muungano zilipokuwa zikishambulia ngome zao na kusababisha vifo vya watu wengi, Alzubidi alitangaza mpito wa miaka miwili kuelekea uhuru, ukiwemo kura ya maoni.

Siku ya Jumatano, STC ilidai kwamba ujumbe wake wa zaidi ya maafisa 50 walikamatwa kiholela na kupelekwa kusikojulikana baada ya kuwasili Riyadh kwa mazungumzo.

(AFPE)

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *