Nimesota Kings Music Records miaka minne hadi natambulishwaNimesota Kings Music Records miaka minne hadi natambulishwa

MSANII wa kwanza wa kike chini ya lebo ya Kings Music Records, Mutimawangu, amesema amepitia safari ndefu na yenye changamoto kwa kukaa kwa miaka minne akisubiri kutambulishwa rasmi na lebo hiyo kabla ya hatimaye kupata nafasi aliyokuwa akiitamani.

Mutimawangu amewasili nchini Tanzania akitokea Rwanda na mara baada ya kutua jijini Dar es Salaam, alizungumza na waandishi wa habari kueleza hisia zake baada ya kutambulishwa rasmi kama msanii mpya wa lebo ya Kings Music Records inayomilikiwa na msanii nyota, Ali Kiba.

Akizungumza na waandishi wa habari, Mutimawangu alisema safari yake ya kusubiri haikuwa rahisi, lakini amekuwa na subira na imani kuwa siku yake ingefika. “Nimekaa benchi kwa muda wa miaka minne nikisubiri kutambulishwa. Haikuwa safari rahisi, lakini ninaamini kila kitu hutokea kwa wakati wake. Leo hii kutambulishwa kama msanii wa kwanza wa kike wa Kings Music ni baraka kubwa kwangu,” alisema Mutimawangu.

Ameongeza kuwa ana matumaini makubwa ya kufanya kazi zenye ubora chini ya lebo hiyo na kuwakilisha vyema wanawake katika tasnia ya muziki, si tu Tanzania bali Afrika Mashariki na kimataifa kwa ujumla. “Niko tayari kufanya kazi kwa bidii, kujifunza na kushirikiana na timu ya Kings Music ili kuhakikisha naleta mchango chanya katika muziki wa Afrika Mashariki,” aliongeza.

Kwa upande wake, msanii na mmiliki wa lebo ya Kings Music Records, Ali Kiba, amesema  uamuzi wa kumtambulisha Mutimawangu umefikiwa baada ya kuona kuwa muda umefika, licha ya changamoto zinazowakabili wasanii wa kike katika safari yao ya muziki. SOMA: Ali Kiba atunukiwa tuzo na wanawake Zanzibar

Ali Kiba amesema tasnia ya muziki ina changamoto nyingi hasa kwa wanawake, hivyo lebo hiyo imejipanga kumpa Mutimawangu ushirikiano na msaada wote unaohitajika ili kufanikisha safari yake ya muziki. “Si rahisi kwa msanii wa kike kudumu na kufanikiwa kwenye muziki kutokana na changamoto mbalimbali. Ndiyo maana Kings Music iko tayari kumpa ushirikiano, malezi na mazingira bora ili aweze kufikia malengo yake,” alisema Ali Kiba.

Ujio wa Mutimawangu chini ya Kings Music Records unaonekana kuwa hatua mpya katika kuimarisha nafasi ya wasanii wa kike ndani ya lebo hiyo na katika tasnia ya muziki kwa ujumla.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *