Diosdado Cabello, Waziri wa Mambo ya ndani wa Venezuela, kupitia televisheni ya taifa ametoa takwimu za waliouawa Jumamosi ikiwa ni mara ya kwanza kwa mamlaka kutoa idadi kamili ya waliopoteza maisha. Awali, jeshi liliorodhesha majina ya wanajeshi 23 pekee waliouawa katika shambulio hilo lililomweka Maduro mikononi mwa Marekani.
Cabello aliyezungumza Jumatano ametuma pia salamu za rambirambi kwa familia za wote waliouawa katika operesheni hiyo Waziri huyo pia amelilaani shambulio la Marekani akisema kuwa, “Venezuela imekuwa mhanga wa shambulio la kikatili ambapo, hadi sasa, watu waliouawa ni 100 na kuna idadi kama hiyo ya majeruhi. Lilikuwa shambulio la kutisha dhidi ya nchi yetu. Huo ni ukweli, ambao hauwezi kufichwa na mtu yeyote, hakuna namna ya kuuficha.”
Waziri huyo amekosoa kuwa kile Marekani inachoifanyia Venezuela inaweza kukifanya pia kwa nchi nyingine. Katika hatua nyingine Rais wa Marekani Donald Trump amesema muda ndiyo utakaoamua kipindi ambacho Venezuela itaendelea kuwa chini ya uangalizi wa nchi yake.
Trump aahidi kuijenga upya Venezuela
Ameyasema hayo katika mahojiano aliyoyafanya na gazeti la New York Times Alhamisi. Amebainisha kuwa Marekani itaijenga upya Caracas na itatumia mafuta ya nchi hiyo, itayachukua na kushusha bei. Aidha Trump amesema ana maelewano mazuri na Rais wa mpito Delcy Rodriguez na ameahidi kuwa taifa lake litaipa Venezuela fedha inayohitajika pakubwa.
Hayo yanaendelea wakati ambapo Trump na kiongozi wa taifa jirani na Venezuela la Colombia, Rais Gustavo Petro wamefanya mazungumzo kwa njia ya simu.
Kupitia ukurasa wake wa jukwaa la Truth Social, Trump amesema Petro alimpigia simu kuelezea hali ya ulanguzi wa dawa za kulevya na tofauti nyingine ambazo viongozi hao wawili wamekuwa nazo. Petro, anayefuata siasa za mrengo wa kushoto amekuwa akikwaruzana na Trump tangu aliporejea madarakani kuiongoza Marekani kwa mara ya pili mwaka uliopita.
Pia Petro alililaani shambulio la Marekani dhidi ya Venezuela na kuuita ukiukwaji wa kuchukiza wa uhuru wa Amerika Kusini uliofanywa na waliozowea kuwafanya wengine watumwa.
Amelifananisha shambulio hilo na la Utawala wa kinazi wa Ujerumani la mwaka 1937 lililoangamiza asilimia 85 ya mji wa Guernica, Uhispania na kuwaua mamia ya watu.