Mamlaka nchini Tanzania, zimetangaza msako dhidi ya waandishi na vyombo vya Habari ambavyo vinafanya kazi bila kuwa na kibali, hatua hii ikilenga kuongeza udhibiti kuhusu uchapishaji wa Habari nchini humo.
Imechapishwa: Imehaririwa:
Dakika 1 Wakati wa kusoma
Matangazo ya kibiashara
Bodi ya uthibiti wa wanahabari nchini Tanzania, JAB, kwenye tarifa yake imesema kuwa wamebaini ongezeko kubwa la watu na vyombo vinavyochapisha habari bila kibali na kwamba wataanzisha operesheni ya nchi nzima kukagua vyombo vya habari kubaini wanaofanya kazi bila idhini.
Taarifa ya bodi imeongeza kuwa ongezeko hili limeshuhudiwa baada ya kumalizika kwa uchaguzi mkuu wa mwezi Octoba mwaka jana, ikiwataka wanaofanya shughuli za uanahabari bila kibali kuacha kufanya hivyo na badala yake wafuate muongozo wa sheria ya huduma za vyombo vya habari ya mwaka 2023.
Tangazo hili limetolewa miezi michache kupita tangu taifa hilo lipitie kipindi kigumu cha machafuko ya baada ya uchaguzi wa Octoba 29, ambapo kulishuhudiwa huduma ya mtandao ikizimwa na mitandao ya kijamii kudhibitiwa.
Katika kipindi hiki mamlaka ziliagiza kufutwa kwa majukwaa na akaunti za mitandao ya kijamii zilizoonekana kukosoa serikali, kitendo ambacho mashirika ya kutetea haki za binadamu ya ndani na nje yalidai uhuru wa vyombo vya habari uliingiliwa kabla, wakati na baada ya uchaguzi.
Hata hivyo pamoja na ukosolewaji bodi ya wanahabari imesema hatua hii haina lengo la kuminya uhuru wa vyombo vya habari na badala yake inataka kuondoa wanahabari makanjanja.