SERIKALI kupitia Wizara ya Uchukuzi imeanza rasmi mchakato wa kuandaa Kanuni za Usimamizi wa Madhara ya Uchovu kwa Madereva za Mwaka 2026. Hatua hiyo inalenga kupunguza ajali za barabarani, kulinda afya za madereva na kuongeza usalama wa abiria na mizigo.

Akifungua kikao cha wadau wa sekta ya uchukuzi Dar es Salaam, Katibu Mkuu wa Wizara ya Uchukuzi, Profesa Godius Kahyarara amesema kanuni hizo zimeandaliwa chini ya Sheria ya Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) Sura ya 413. Profesa Kahyarara amesema kanuni hizo zinakusudia kuweka mwongozo wa kitaifa kuhusu saa za kazi, mapumziko ya lazima na utaratibu wa kubadilishana madereva, hususan kwa safari za masafa marefu.

Amesema ongezeko la shughuli za usafirishaji nchini linalochangiwa na nafasi ya Tanzania kama lango la biashara kwa nchi zaidi ya nane za kanda, pamoja na kuruhusiwa kwa mabasi ya masafa marefu kufanya kazi saa 24, limeongeza umuhimu wa kuwa na kanuni mahususi za kudhibiti uchovu wa madereva. Kuhusu ujenzi wa miundombinu ya barabara, Profesa Kahyarara alisema kwa mwaka 2024 mtandao wa barabara nchini ulifikia kilometa 181,864.81, huku usajili wa vyombo vya usafiri ukiongezeka kwa kasi.

Profesa Kahyarara amesema malori 201,388 yalipewa leseni mwaka 2024 ikilinganishwa na 183,392 mwaka 2023, wakati mabasi ya masafa marefu na mafupi yaliongezeka kutoka 50,316 mwaka 2023 hadi 64,635 mwaka 2024. Kwa mujibu wake, changamoto kuu zilizolazimisha kuandaliwa kwa kanuni hizo ni kukosekana kwa mfumo wa kisheria wa kudhibiti uchovu wa madereva, ongezeko la ajali zinazohusishwa na uchovu na uhitaji wa kulinda afya na ustawi wa madereva.

Kanuni hizo pia zinawataka wamiliki wa vyombo vya usafiri kuandaa mpango wa usimamizi wa madhara ya uchovu, pamoja na kuweka wajibu wa moja kwa moja kwa madereva kuzingatia muda wa kazi na mapumziko. “Tunaamini utekelezaji wake utaongeza ubora na usalama wa huduma za usafiri wa barabarani,” alisema

Profesa Kahyarara. Aidha, LATRA imeendelea kuimarisha usimamizi wa sekta kwa kutumia teknolojia ikiwamo mifumo ya ufuatiliaji wa vyombo (VTS), vifaa vya utambuzi wa madereva (i-buttons), pamoja na matumizi ya Tiketi Mtandao na Safari Tiketi App ili kuboresha uwazi na usalama wa safari.SOMA: Ajali za barabarani zapungua kwa asilimia 35 Geita

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *