Vijana 1,432 wapata ajira nje ya nchiVijana 1,432 wapata ajira nje ya nchi

SERIKALI imewapatia vijana wa Tanzania 109 ajira za nje ya nchi na kufanya idadi ya vijana waliopata ajira kuanzia Desemba 2025 hadi Januari 2026 kufi kia 1,432. Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Ajira na Mahusiano, Deus Sangu alieleza hayo wakati wa hafla ya kuwaaga vijana hao 109, baada ya kumaliza mafunzo ya muda mfupi ya ajira za nje ya nchi iliyofanyika Dar es Salaam.

Vijana hao watakwenda kufanya kazi za ufundi umeme, ujenzi, madereva wa malori ya mizigo, wahudumu wa maabara, wasaidizi wa kazi za ndani na maofisa kilimo katika nchi za Oman, Denmark, Saudi Arabia, Qatar na Falme za Kiarabu (UAE).

Sangu amesema ajira hizo ni matokeo ya utendaji kazi wa Serikali ya Awamu ya Sita katika kuendelea kuboresha, kuimarisha mazingira na mifumo ya upatikanaji wa ajira, kuongeza ulinzi wa kisheria wa ufanyaji kazi nje ya nchi na kutoa mafunzo kwa vijana kabla ya kuondoka kwenda nje ya nchi, na kukuza ushirikiano na nchi mbalimbali.

Amesema ajira hizo zimepatikana kutokana na juhudi za Rais Samia Suluhu Hassan za kuimarisha mahusiano ya kidiplomasia ambayo yameleta fursa za ajira kwa vijana. Sangu amesema katika kudhihirisha hilo, hivi karibuni Rais Samia alimuagiza Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mahmoud Thabit Kombo kushughulikia suala la ajira kimataifa, ikiwamo walizozipata vijana hao.SOMA: Uwekezaji Bandari ya Tanga wazaa matunda, fursa lukuki

“Bado kuna fursa 8,000 zinakuja na serikali inaendelea na mchakato wa kuzungumza na mataifa mengine kwa ajili ya vijana wetu kufanya kazi nje ya nchi, na tuna ajira 500 tulizozitangaza hivi karibuni kwa madereva pikipiki, ndio maana tunasema ajira hizi zinagusa makundi yote ya vijana,” alibainisha Sangu.

Amesema serikali itaendelea kushirikiana na mawakala wa ajira nchini kuhakikisha ajira za kimataifa zinapatikana na Watanzania wanaenda kufanya kazi nje ya nchi zenye staha, haki na kutokana na miongozo ya ajira za kimataifa.

Ameongeza kuwa Tanzania imeunda makubaliano ya pamoja na nchi mbalimbali kutafuta fursa za kuwaongezea ujuzi na ajira vijana wa Tanzania. Miongoni mwa nchi hizo ni Japan ambayo wanajadiliana sekta ya ujenzi inayotaka kuwaandaa vijana zaidi ya 5,000 watakaokuwa na uwezo wa kujenga majengo makubwa na imara.

Ameagiza ajira zote za kimataifa zinazotolewa na serikali kuwafikia vijana wa nchi nzima kuanzia ngazi ya kata, kijiji na mkoa. “Hivi karibuni tumepata tena fursa za kazi 10,000 katika nchi ya Saudi Arabia, wauguzi wanaofanya kwenye hospitali ya serikali na kada nyingine ambazo zinahitaji wale wenye ujuzi na wasio na ujuzi,” alisema Sangu.

Amewataka vijana hao 109 kuheshimu sheria na tamaduni za nchi wanazokwenda, kufanya kazi kwa bidii, kuwa wazalendo na nidhamu ya fedha ili watakaporudi wakawe mfano kwa vijana wengine wenye shaka ya kufanya kazi kama hizo.

“Mnakwenda ugenini mmeacha familia, wazazi na watoto. Jambo kubwa ni nidhamu, ndio maana tutakuwa na nyie kuhakikisha hampati manyanyaso… Haki zenu zitalindwa, nanyi mna wajibu wa kuitangaza Tanzania kwa sababu mmebeba sura ya nchi. Hivyo, mkaitangaze vyema Tanzania kuanzia kwenye mila, desturi na rasilimali zetu,” alieleza Sangu.

Amesema serikali inatarajia kutangaza ajira nyingine 1,000 mwishoni mwa Januari kwa madereva malori, mabasi, mafundi magari na mafundi viyoyozi, ikiwa ni utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 inayoelekeza kujenga uchumi shindani na himilivu utakaoleta ajira na fursa kwa vijana na Watanzania.

Naye Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Ajira na Wenye Ulemavu), Zuhura Yunus alisema dhamira ya ajira hizo ni kuthibitisha kwa vitendo dhamira ya serikali kuhakikisha uhamaji wa nguvukazi unafanyika kwa mpangilio kwa kuzingatia haki, usalama na ustawi wa Watanzania wanaofanya kazi nje ya nchi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *