Kwa mujibu wa Taasisi ya Wahandisi wa Kenya takribani asilimia 80 ya majengo yaliyopo jijini Nairobi ni hatari kwa usalama, na asilimia 80 ya majengo yanayoendelea kujengwa kote nchini humo hayajafanyiwa ukaguzi.

Kauli hizo zinajiri siku chache baada ya jengo la ghorofa 14 lililokuwa likijengwa katika eneo la South C jijini Nairobi kuporomoka na watu wanne walikufa kwenye maafa hayo. Uchunguzi wa awali umebaini kuwa jengo hilo mara kadhaa lilikuwa limewekewa alama ya hatari lakini ujenzi haukusitishwa uliendelea.

Nairobi yawa kitovu cha majaribio ya uzembe na tamaa

Tukio hilo limeibua hasira za umma na maswali mazito kuhusu uwajibikaji wa maafisa wa kaunti na wadau wa sekta ya ujenzi. Rais wa Taasisi ya Wahandisi nchini Fawcett Omollo, amesema takwimu hizo zinaakisi kwa uwazi kushindwa kwa mifumo ya udhibiti na usimamizi wa ujenzi, akionya kuwa Nairobi imegeuka kuwa eneo la majaribio ya uzembe na tamaa.

Kenya Nairobi | Jengo kuanguka
Wahudumu wa dharura wa Kaunti ya Nairobi, wafanyakazi wa Msalaba Mwekundu wa Kenya na Shirika la Misaada la Poland wanatafuta watu wanaohofiwa kukwama chini ya jengo la makazi lililoporomoka katika eneo la makazi la Kahawa West jijini Nairobi mnamo Oktoba 20, 2024.Picha: LUIS TATO/AFP

Alisema “Mtetemeko mdogo wa ardhi ukitokea majengo mengi yataporomoka, kwenye majimbo yetu kama vile Nairobi, washauri hulazimishwa kuidhinisha majengo kuwa salama, hivyo kuwaondolea lawama maafisa husika wa majimbo lawama.”

Wahandisi sasa wanaitaka serikali ya kitaifa na za kaunti kuchukua hatua kali, ikiwemo kusimamisha mara moja miradi isiyofuata viwango kuwawajibisha maafisa wanaotoa vibali kiholela na kuhakikisha kuwa ni wataalamu walioidhinishwa pekee wanaohusika katika miradi ya ujenzi. Kwa mujibu wao, janga la South C linapaswa kuwa ishara ya mwisho ya onyo, kabla jiji la Nairobi halijageuka kuwa eneo la mauti.

Uzembe umeathiri pakubwa sekta ya ujenzi

Kwa upande wake, Rais wa Wataalamu wa Usanifu majengo wa Taifa, Sylvia Kasanga, amesema sekta ya ujenzi imekuwa ikikumbwa na matukio ya uzembe unaoanzia kwenye usanifu, kuidhinishwa kwa michoro hadi usimamizi wa kazi halisi.

Kenya Nairobi | Watu wakiwa wamesimama nje ya majengo wakitazama waandamanaji waliokuwa wakipinga gharama ya maisha | Wakazi
Watu wakiwa nje ya jengo wakitazama wafuasi wa kiongozi wa upinzani wa Kenya Raila Odinga wa Azimio La Umoja (Azimio la Umoja) One Kenya Alliance, wakishiriki katika maandamano ya kitaifa kupinga kupanda gharama ya maisha, Nairobi, Kenya Machi 27, 2023.Picha: Monicah Mwangi/REUTERS

“Inasikitisha tumepoteza maisha ambayo hatukustahili kuyapoteza, kwani tumewekeza kwa wataalamu wengi tu, tunateta sababu wasanifu majengo wengi, wahandisi wengi tu hawana kazi.,” alisema Kisanga.

Wakati huo huo Kitengo cha Kitaifa cha Usimamizi wa Majanga kimehitimisha operesheni ya utafutaji, uokoaji na kurejesha miili katika jengo lililoporomoka South C, ambapo miili minne ilipatikana.

Kamanda wa Tukio na Mkurugenzi wa Kitengo hicho Dkt. Duncan Onyango Ochieng, amesema kuwa malengo yote muhimu ya operesheni ya dharura yametimizwa, jambo linaloashiria ukomo wa shughuli za dharura katika eneo la jengo la ghorofa 14 lililoporomoka. Yamkini majengo 80 yameporomoka katika kipindi cha miaka mitano nchini Kenya, hali inayoonyesha kuwa tatizo linaendelea kuongezeka badala ya kupungua.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *