
Mechi hiyo ilikuwa ni ya robo fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika kati ya Algeria na Nigeria
“CAF imeliwasilisha suala hilo kwa bodi ya nidhamu kwa ajili ya uchunguzi na kutoa wito wa kuchukua hatua zinazofaa ikiwa muhusika atakutwa na hatia kwa kufanya kosa,” limesema shirikisho hilo la soka Afrika kwenye taarifa yake.
Kulishuhudiwa sekeseke uwanjani mwishoni mwa mechi hiyo iliyochezwa siku ya Jumamosi mjini Marrakesh, ambapo Nigeria ilishinda 2-0, ushindi uliopatikana kufuatia magoli ya kipindi cha pili cha mchezo yaliyofungwa na Victor Osimhen na Akor Adams.
Hatua zozote za kinidhamu zinaweza kuwa na athari kwa timu ya Super Eagles, wakati wakijiandaa na mchezo wa nusu fainali siku ya Jumatano dhidi ya Morocco.
Hata hivyo, CAF imesema inachunguza pia matukio yaliyotokea katika mchezo wa robo fainali siku ya Ijumaa kati ya Morocco na Cameroon
Morocco ilishinda mchezo huo kwa 2-0 mjini Rabat, lakini Indomitable Lions hawakufurahishwa na refa na hasa baada ya kunyimwa penati baada ya Bryan Mbeumo kuchezewa rafu katika nusu ya pili ya mchezo. Mbeumo anaichezea pia Manchester United ya England.