TANGA: Watu wanne wamepoteza maisha kufuatia ajali ya kugongana uso kwa uso kati ya magari mawili, iliyotokea katika eneo la Mkumbara, Tarafa ya Mombo, wilayani Korogwe, kwenye barabara kuu ya Same–Korogwe.

Ajali hiyo imesababisha taharuki kubwa kwa wakazi wa eneo hilo na wasafiri waliokuwa wakitumia barabara hiyo muhimu inayounganisha mikoa ya Tanga, Kilimanjaro, na Arusha, huku shughuli za usafiri zikiathirika kwa muda.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga, ACP Alimachius Mchunguzi, ajali hiyo ilitokea majira ya saa 9:30 asubuhi, ikihusisha gari la mizigo aina ya Scania lenye namba za usajili T 812 ELQ, lililokuwa limeunganishwa na trela yenye namba T 106 DGS, mali ya kampuni ya Mikoani Edible Oil and Detergents Ltd, likitokea Same kuelekea Korogwe.

Taarifa hiyo imeeleza kuwa gari hilo la mizigo liligongana uso kwa uso na basi aina ya Yutong lenye namba ya usajili T 579 ECH, mali ya kampuni ya Mwensino, lililokuwa likitokea wilayani Lushoto kuelekea mkoani Arusha.

Polisi wamebainisha kuwa mmoja wa marehemu ni Hazbadir Iddy, mwenye umri wa miaka 30, mkazi wa Goha wilayani Lushoto na fundi wa magari, aliyekuwa miongoni mwa waliokuwa kwenye vyombo hivyo.

Wanaume wengine watatu waliopoteza maisha bado hawajatambuliwa, huku taratibu za kuwatambua zikifanyika kwa kushirikiana na ndugu zao na vyombo husika.

Katika ajali hiyo, watu 16 wamejeruhiwa, wakiwemo madereva wa vyombo hivyo pamoja na abiria. Wote wamekimbizwa Kituo cha Afya Mombo kwa matibabu, huku miili ya marehemu ikihifadhiwa kwa taratibu zinazofaa.

Jeshi la Polisi Mkoa wa Tanga linaendelea na uchunguzi wa ajali hiyo, huku likiwataka madereva kuzingatia sheria za usalama barabarani, kuepuka mwendo kasi, uzembe, na maamuzi hatarishi ili kuzuia ajali zinazoweza kuepukika.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *