
CAF imechukua hatua hiyo kufuatia kile lilichosema ni “tabia zisizokubalika”.
Hii ni baada ya wachezaji kupigana uwanjani mwishoni mwa mchezo wa robo fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON 2025) kati ya Algeria na Nigeria.
CAF imesema katika taarifa kuwa imewasilisha suala hilo kwa bodi ya nidhamu kwa ajili ya uchunguzi na kutoa wito wa kuchukua hatua zinazofaa. Kulishuhudiwa sekeseke uwanjani mwishoni mwa mechi hiyo iliyochezwa Jumamosi mjini Marrakesh, ambapo Nigeria ilishinda 2-0, ushindi uliopatikana kufuatia magoli ya kipindi cha pili cha mchezo yaliyofungwa na Victor Osimhen na Akor Adams.
Hatua zozote za kinidhamu zinaweza kuwa na athari kwa timu ya Super Eagles, wakati wakijiandaa na mchezo wa nusu fainali siku ya Jumatano dhidi ya Morocco. Hata hivyo, CAF imesema inachunguza pia matukio yaliyotokea katika mchezo wa robo fainali siku ya Ijumaa kati ya Moroccona Cameroon.
Morocco ilishinda mchezo huo kwa 2-0 mjini Rabat, lakini Indomitable Lions hawakufurahishwa na refa na hasa baada ya kunyimwa penati baada ya Bryan Mbeumo kuchezewa rafu katika nusu ya pili ya mchezo.