
“Jeshi linafanyia hali tathmini, na tunaangalia njia thabiti. Tutafanya maamuzi,” Trump aliwaambia waandishi wa habari akiwa kwenye ndege ya rais wa Marekani ya Air Force One kuelekea Washington, DC, kutoka Mar-a-Lago, Florida.
Trump pia alisema amekuwa akipata taarifa za kila saa kuhusu Iran, bila kueleza zaidi kuhusu wakati gani, wapi, na namna gani Marekani itachukua hatua.
Maandamano ya Iran
Iran imekumbwa na maandamano tangu mwishoni mwa mwezi Disemba kutokana na hali mbaya ya kiuchumi inayokithiri.
Shirika la haki za binadamu lenye makao yake nchini Marekani la HRANA linasema waliofariki ni waandamanaji 490 na maafisa wa usalama 48, huku watu zaidi ya 10,600 wakikamatwa, ingawa hakuna makadirio rasmi kuhusu idadi hiyo.
Mwezi Juni mwaka uliopita, Marekani ilishambulia maeneo matatu ya kutengeneza nyuklia ya Iran — Fordow, Natanz, na Isfahan — ikiwa ni sehemu ya operesheni yao ya Midnight Hammer wakati wa vita vya muda mfupi vya Iran na Israel.
Pamoja na kutoa onyo kuhusu hatua za kijeshi, Trump amesema anaangalia njia za kurejeshwa kwa huduma za mtandao Iran huku zikiwa zimekatishwa kote, akisema kuwa atazungumza na Elon Musk kuhusu hilo.