‘Serikali ya Tanzania iliua kiholela wakati wa uchaguzi’‘Serikali ya Tanzania iliua kiholela wakati wa uchaguzi’

Ripoti iliyotolewa Jumatatu inasema kuwa vikosi vya usalama vya Tanzania vilifyatua risasi dhidi ya waandamanaji waliokuwa wakikimbia na kufanya mauaji ya “mtindo wa kunyonga” wakati wa machafuko ya uchaguzi mwaka jana Ripoti hiyo ilithibitisha picha zilizosambaa mitandaoni kwa kutumia pia picha za droni na satelaiti.

Ripoti hiyo imetolewa na Centre for Information Resilience (CIR), shirika huru lenye makao yake nchini Uingereza linalofanya uchunguzi wa kidijitali. Shirika hilo lilikusanya na kuchambua ushahidi wa machafuko yaliyozuka wakati wa uchaguzi wa Oktoba 29 nchini Tanzania.

Maandamano yenye vurugu yalizuka baada ya serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan kushutumiwa kwa kuwazuia wapinzani wake wakuu kugombea na kwa kutekeleza mfululizo wa utekaji nyara na mauaji kabla ya uchaguzi.

Upinzani unasema takribani watu 2,000 waliuawa na vikosi vya usalama katika siku chache za machafuko, hali ambayo ilikuwa vigumu kuithibitisha kwa sababu serikali iliwazuia waandishi wa habari wa kigeni kuingia nchini ikaweka marufuku ya kutotoka nje, na kuzima kabisa huduma za intaneti kwa siku kadhaa.

Rais Samia alishinda kwa asilimia 98 ya kura

Rais Samia Suluhu Hassan alitangazwa mshindi wa uchaguzi kwa asilimia 98 ya kura Alitetea mauaji hayo akisema yalikuwa muhimu kuzuia kupinduliwa kwa serikali, na akadai kuwa hakuna nguvu kupita kiasi iliyotumika.

Tansania Dodoma 2025 | Rais Samia Suluhu Hassan akila kiapo cha kuwa rais
Pichani anaonekana Rais Samia Suluhu Hassan wakati wa kuapishwa kwake mjini Dodoma, Tanzania. Mahali: Dodoma, Tanzania. Tarehe: Novemba 3, 2025. Hakimiliki: Tanzania State Press.Picha: Tanzania State press

Hata hivyo, CIR ilichambua picha na video 185 zilizorekodiwa kati ya Oktoba 29 na Novemba 4, kipindi ambacho marufuku ya kutotoka nje iliondolewa, pamoja na picha za satelaiti na video za droni. Ripoti hiyo ilisema CIR “ilithibitisha matumizi ya mara kwa mara ya risasi za moto na vikosi vya usalama pamoja na wanaume wenye silaha waliovaa nguo za kiraia, hali iliyosababisha vifo na majeruhi.”

Ripoti hiyo pia “ilibaini uwezekano wa makaburi ya halaiki kupitia picha za satelaiti na kuthibitisha uwepo wa marundo makubwa ya miili” katika maudhui yaliyotengenezwa na raia, pamoja na picha zinazoonyesha raia “wakishambuliwa” na “kudhalilishwa”.

Aidha, CIR ilitoa ramani ya matukio ambapo ilithibitisha picha za waandamanaji “wakiharibu majengo, wakichoma moto, na kuwarushia mawe maafisa wa polisi”.

“Ufyatuaji wa risasi bila kuchagua”

Ushahidi huo unajumuisha video zilizothibitishwa za “kupigwa risasi kwa waandamanaji waliokuwa wakikimbia, akiwemo mwanamke mjamzito, karibu na barabara kuu ya A104” jijini Arusha. Pia kuna picha za usiku kutoka Mwanza zinazoonyesha “mauaji ya mtindo wa kunyonga yaliyotekelezwa mbali na maeneo makuu ya maandamano”.

Katika tukio moja, video ya droni ya Dar es Salaam iliyotolewa kwa CIR inaonyesha “gari jeupe likiwafukuza raia, kabla ya waliokuwa ndani yake kushuka na kuanza kufyatua risasi kiholela kuelekea nyumba za karibu”.

Hotuba ya Samia baada ya kuapishwa

To view this video please enable JavaScript, and consider upgrading to a web browser that supports HTML5 video

Serikali ya Tanzania haikujibu maombi ya mara kwa mara ya kutoa maoni yaliyotumwa na shirika la habari la AFP.

AFP pia ilimnukuu daktari katika hospitali kubwa jijini Dar es Salaam aliyesema kuwa mamia ya wagonjwa waliojeruhiwa na maiti ziliondolewa katika hospitali hiyo na kupelekwa maeneo ya siri wakati wa kilele cha machafuko.

CIR ilibaini ushahidi wa udongo uliovurugwa hivi karibuni kati ya Novemba 2 na 5 katika makaburi ya Kondo karibu na Dar es Salaam—eneo ambalo afisa mmoja mwandamizi wa serikali, aliyekerwa na ukandamizaji huo, aliambia AFP huenda lilitumika kama kaburi la halaiki. Eneo hilo pia lilitambuliwa katika uchunguzi wa CNN.

Picha za satelaiti za CIR pia zilionyesha ujenzi wa miundombinu ya muda katika Hospitali ya Wilaya ya Kivule jijini Dar es Salaam wakati wa machafuko, hali inayounga mkono ripoti kuwa jengo la muda la kuhifadhia maiti lilijengwa haraka kushughulikia idadi kubwa ya vifo. Dalili za uwezekano wa kaburi jingine la halaiki pia zilibainishwa katika Chuo cha Kilimo cha Tengeru jijini Arusha.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *