Baadhi ya waangalizi wamelalamika kwamba hatua hiyo ya tume inalenga kubana uhuru wao wa kueleza waziwazi kilichotokea wakati wa uchaguzi. Kama ilivyo katika nchi mbalimbali, waangalizi wa kigeni wanaoalikwa na serikali ya Uganda kusimamia uchaguzi, wamekuwa sehemu ya muundo wa kufuatilia zoezi hilo kuhakiki viwango vya kuwa huru na haki.
Hata hivyo maagizo ambayo waangalizi wamepewa na tume ya uchaguzi ikiwa pamoja na vyombo vya usalama vya nchi hiyo yanashiria kuwa safari hii wataendesha shughuli zao chini ya masharti tofauti na walivyotarajia. Kwa mfano waangalizi wameagizwa kutowasilisha ripoti zao kwa umma wala vyombo vya habari kabla ya kuziwasilisha kwa tume hiyo.
Mwenyekiti wa Tume hiyo Jaji Simon Byabakama ametamka hivi kwenye kikao cha kutoa maelekezo kwa waangalizi. “Kutokana na hali ambayo tumewahi kukumbwa nayo hapo awali, waangalizi wasitoe ripoti zao kwa umma kabla ya kuziwasilisha kwa tume ya uchaguzi. Hii ni kwa sababu tunataka kuwepo mchakato unaoaminika kufanyika katika mazingira ya usawa na amani.”
Tamko hili limeibua hoja kama tume ya uchaguzi ndiyo itakayoidhinisha ripoti za waangalizi Katika chaguzi zilizopita ujumbe wa ngazi za juu ukijumlisha waangalizi kutoka jumuiya na mashirika mbalimbali ya utawala na demokrasia wamekuwa wakija Uganda kufuatilia hali ya uchaguzi kabla wakati na baada ya zoezi la kupiga kura.
Kisha wao hutoa taarifa kuhusu walichoshuhudia kwa mujibu wa uchaguzi kuwa wa kidemokrasia yaani huru na haki na pia wenye uwazi katika hatua ya kuhesabu na kutangaza matokeo. Katika ripoti zao wajumbe hao aidha hutoa mapendekezo kuhusiana na mapungufu yaliyojitokeza na kuyawasilisha kwa serikali. Balozi Dkt Deo Mwapinga ambaye ni katibu mkuu wa jukwaa la kibunge la nchi za maziwa makuu ICGLR lenye makao yake makuu Kinshasa ameelezea kile watachozingatia kufuatia maelekezo hayo
Amesema “Sisi tupo hapa si kwa ajili ya kuwa marefa.Tumekuja kuangalia na hiki kilikwenda hivi au vile. Si kusema kwamba hapa umepiga buti. Tumekuja kuangalia kama zile sheria za nchi yenu kama Waganda mnazifuata.”
Kulingana na baadhi ya wadadisi wa masuala ya kisiasa, masharti waliowekewa waangalizi yanazidi kuthibitisha kwamba wao ni watalii wa uchaguzi na hawana mchango wowote watakaotoa kwa mchakato wa kidemokrasia na utawala wa kisheria.wanazidi kufahamisha kuwa kiwango cha chini cha ushiriki wa waangalizi wa Umoja wa Ulaya ni kielelezo kuwa mataifa hayo hayaoni haja ya kujigharimu muda na fedha zao kwani hata mapendekezo wanayotoa kila baada ya uchaguzi kama vile kuepuakana na kukandamiza upinzani katika kipindi cha kampeni hayatiliwi maanani.
Mchambuzi Moday Akol Amazima amesema “Waangalizi kuitwa watalii wa uchaguzi ni kwamba hata pale wanapopewa masharti yanayokiuka kanuni msingi za uchaguzi bora, hawapingi na kusema hapana sisi hatutaendelea Basi tunarudi makwetu.”
Makundi ya waangalizi yanajumuisha ujumbe za Umoja wa Afrika ukiongozwa na aliyekuwa rais wa Nigeria Goodluck Jonathan ambaye amehimiza kuwepo na fursa kwa mataifa kama Uganda kubadilisha uongozi wa njia ya amani.
