Vifo huripotiwa mara kwa mara, na baadhi ya wakimbizi wamesema wanataka kurudi katika nchi zao.
Katika kambi ya Bikinga iliyoko nchini Burundi, kuna maelfu ya familia za wakongomani walioomba hifadhi Walikimbia vita na kukhofia usalama wao. Licha ya kupata usalama lakini hapa kumekuwa na hofu nyingine kama anavyosema Hasha Alima.
Hasha Alima, mkimbizi kutoka Kongo aliyepo kwenye kambi ya Bikinga amesema “Walitupakiza kwenye magari na wakatuleta katika kambi tunahangaika na kukosa chakula baridi ni kali sana na watoto hawana kitu cha kujifunika. Tulikimbia kifo Kongo lakini njaa ndio itatuuwa hapa.”
Mashaka Kukwa, naye ni mkimbizi na baba wa watoto 7. Yeye anasema anaipenda nchi yake Kongo na anatamani viongozi warejeshe amani ili aweze kurejea nyumbani.
“Naipenda nchi yangu siwezi rudi haraka sababu bado kuna vita. nataka viongozi kutafuta na kupata suluhu kwa hili maana tunahishi katika mateso,” anasema mkimbizi huyo.
Serikali ya Kongo yatoa ujumbe wa matumaini
Serikali ya Kongo, kupitia Waziri wa Masuala ya Jamii, Eva Bazaiba Masudi ilifanya ziara ya dharura ya saa chache nchini Burundi, ambapo alikutana na wakimbizi, kuwapa pole na kuwapa ujumbe wa matumaini.
”Kwa niaba ya Serikali ya Kongo, tuko hapa kuwafariji, kwa sababu kilichowafika kimetufika sote. Tuko hapa kwa sababu ninyi ni watu muhimu, na kilichotokea kinatugusa sisi sote. Tunasubiri na tunajitahidi kurejesha amani, na tunasikitika sana kwa mateso mnayopitia. Hivyo basi, tafadhali muelewe kuwa hatua ndogo tiliyoichukua leo si kwa ajili ya kupunguza uzito wa mateso yenu tu, bali kutaka kuwapa furaha,” alizema Bazaiba.
Zaidi ya wambizi 250,000 walikimbilia nchini Burundi na zaidi ya 100,000 nchini Tanzania. Wote wakitokea Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Kongo walivuka mipaka na kukimbilia nchini Burundi baada ya mapigano kutoka kwa waasi wa M23 dhidi ya jeshi la Kongo FARDC pamoja na Wanamgambo wa raia wenye hasira na wanaopania kuilinda nchi yao kama wazalendo. Tayari Zaidi ya wakimbizi 105 wanaripotiwa kufariki kutokana na magonjwa ya kuharisha pamoja na njaa.