MWANZA: Wananchi wa mtaa wa National, kata ya Nyakato wilayani Ilemela, mkoani Mwanza wameshauri kuwepo wa mikutano ya hadhara kila mwezi, kufahamishwa serikali imewafanyia shughuli zipi kimaendeleo.
Wito huo umetolewa katika mkutano wa hadhara, baada ya diwani wa kata hiyo, Jonathan Mkuba, kuwaeleza kwamba Zahanati ya Nyakato imeshaanza kutoa huduma zenye hadhi ya kituo cha afya, kuanzia Oktoba, 2025.

“Tunapaswa kutambua serikali inafanya nini kwa kwa ajili ya wananchi wake. Hii itapunguza lawama za watawaliwa dhidi ya watawala.
“Kwa kutofahamu, bado tumekuwa tukifuata huduma hasa za kujifungua Kata nyingine katika kituo cha afya ya Buzuruga, wakati kumbe zipo hapa mtaani kwetu,” amesema Rebeca Gervas, kwa niaba ya wenzake, huku akiipongeza serikali kwa hatua hiyo.

Diwani ameeleza kwamba upanuzi huo uliokamilka mwaka jana, ulihusisha pamoja na mambo mengine, ujenzi wa jengo la mama na mtoto pamoja na wodi ya wanawake.
“Mradi huo ulizinduliwa na Mwenge wa Uhuru mwaka jana. Na upanuzi unaendelea kwani hivi karibuni tutaanza ujenzi wa jengo la upasuaji hapa,” alisema Diwani huku akitoa fursa ya wananchi kuingia kwenye majengo mapya kujionea miundombinu iliyomo.