Iran iliwaruhusu raia kupiga simu za kimataifa kupitia simu zao za mkononi siku ya Jumanne. Hata hivyo, haikupunguza vizuizi vya mtandao wala kuruhusu huduma za kutuma ujumbe kurejeshwa. Haya yanajiri mnamo wakati idadi ya waliouawa katika maandamano ya siku kadhaa yaliyogubikwa na umwagaji damu ikidaiwa kupanda hadi watu 646.
Watu kadhaa mjini Tehran waliweza kuwapigia simu waandishi wa shirika la habari la Associated Press na kuzungumza nao. Aidha waandishi habari wa shirika hilo walioko Dubai huko Umoja wa Falme za Kiarabu pia waliweza kuwapigia simu na kuzungumza nao.
Kulingana na mashahidi, hatua hiyo imeleta unafuu kidogo baada ya mitandao na mawasiliano yote kuzimwa kwa siku nne na nusu zilizopita. Wameelezea kuona idadi kubwa ya maafisa wa usalama Katikati ya mji mkuu Tehran.
Hata hivyo, mashahidi wamesema wanaweza kuzipata tovuti rasmi za serikali ndani ya nchi kupitia intaneti lakini bado intaneti imeminywa wasiweze kuperuzi mitandao ya nje ya nchi.
Maandamano Iran yatishia utawala wa Ayatollah Ali Khamenei?
Iran imetikiswa na maandamano makubwa yaliyochochewa na hali ngumu ya kiuchumi. Lakini ambayo yamebadilika kuwa mtihani mkubwa kiusalama na tishio kwa utawala wa Jamhuri hiyo ya Kiislamu. Hata hivyo Khamenei amekuwa akikosoa maandamano dhidi ya serikali.
Serikali ya Tehran imelaumiwa pakubwa kwa kutumia nguvu kubwa kuwakandamiza waandamanaji hao, ambao baadhi wamesikika wakimtaka kiongozi mkuu wa kidini wa taifa hilo Ayatollah Ali Khamenei ang’atuke madarakani.
Makundi ya kutetea haki za binadamu yameripoti kuwa idadi ya watu waliouawa hadi sasa imezidi 600, miongoni mwao wakiwa waandamanaji 512 na 134 wakiwa maafisa wa usalama.
Kulingana na wanaharakati ambao makao yao makuu yako Marekani, zaidi ya watu 10,700 wamekamatwa.
Jumuiya ya kimataifa yalaani ukandamizaji wa maamndamano Iran
Ukandamizaji wa waandamanaji nchini Iran umelaaniwa ndani na nje ya nchi hiyo ya Mashariki ya Kati.
Kansela wa Ujerumani, Friedrich Merz, alisema Jumanne kwamba utawala wa Iran unaishi siku zake za mwisho.
Uhispania umemuita balozi wa Iran aliyeko Madrid, kuelezea kughadhabishwa kwake na pia kulaani vitendo vya serikali ya Tehran dhidi ya waandamanaji.
Hapo awali utawala wa Trump ulitishia kuingilia kati kijeshi endapo Iran ingekandamiza maandamano. Lakini siku ya Jumatatu, Rais Trump alisema Iran ilitaka mazungumzo baada ya kitisho chake cha kuishambulia Iran kujibu ukandamizaji wake.
“Lakini tunatathmini kwa undani. Jeshi linafanya tathmini, na tunatafakari mbinu nyingine mbadala zenye nguvu. Tutafanya maamuzi,” amesema Trump.
Trump atangaza ushuru kwa washirika wa Iran kibiashara
Jana Jumatatu, Rais Donald Trump alitangaza ushuru wa asilimia 25 kutoka Marekani kwa nchi zinazofanya biashara na Iran. Trump alitangaza ushuru huo katika chapisho la mitandao ya kijamii, akisema “utaanza kutumika mara moja.”
Hatua hii inalenga kuiongezea Iran shinikizo endapo washirika wake wakuu kibiashara ikiwemo Brazil, China, Uturuki, Umoja wa Falme za Kiarabu na Urusi zitasitisha biashara.
Iran kupitia Waziri wake wa Mambo ya nje Abbas Araghchi, imesema tayari inazungumza na Washington kupitia mjumbe wake maalum Steve Witkoff. Aidha siku ya Jumatatu, Araghchi alisema nchi yake iko tayari kwa vyote viwili, vita na mazungumzo kati yao na Marekani.
(APE; AFPE;APTN)