RAIS mstaafu Jakaya Kikwete amesema Zanzibar ya zamani ni tofauti na ya sasa kutokana na mabadiliko makubwa ya kimaendeleo yaliyofanyika, ikiwemo ujenzi wa kiwanja cha ndege na mabadiliko hayo yametokana na mapinduzi ambayo jana yamefikisha miaka 62.
Kikwete aliyasema hayo wakati akifanya mahojiano na Kituo cha Televisheni cha TBC.
Alisema maendeleo yanayopatikana sasa yanatokana na uongozi unaopenda matokeo, akitolea mfano ujenzi wa madaraja ya juu pamoja na majengo ya ghorofa.
SOMA: Kasi ya maendeleo Zanzibar uhalisia Mapinduzi ya 1964
Alisema majengo ya mwisho makubwa kujengwa kabla ya hapo yalikuwa ni yale ya Michenzani yaliyojengwa na Abeid Amani Karume, na tangu kifo chake mwaka 1972 hakukuwa na majengo mapya makubwa zaidi ya kukamilisha yale yaliyoachwa.
Kikwete alisema maendeleo makubwa yanayoonekana sasa yanajumuisha ujenzi wa Kiwanja cha Ndege cha Abeid Amani Karume ambacho kwa sasa kinapokea wageni wengi, kiwanja cha ndege cha Pemba, ujenzi wa hoteli nyingi na ongezeko la watalii, hali inayofanya Zanzibar ivutie zaidi.
Akizungumza kuhusu Dk Hussein Mwinyi, Kikwete alisema ni kiongozi mwenye maono na mtazamo wa kisasa kuhusu Zanzibar yenye maendeleo, na ni mtu makini anayejipa muda wa kufikiri kabla ya kufanya maamuzi, ilihali ni kizazi cha baada ya Mapinduzi.
Alisema wakati wa uongozi wake, Dk Mwinyi alipokuwa Waziri wa Ulinzi, alimuomba ajiuzulu nafasi hiyo baada ya mlipuko wa mabomu ya Mbagala, lakini alikataa.
“Kukataa kwangu ni kwa sababu hakukuwa na mtu wa kulaumiwa. Katika ghala lile lililokuwa linahifadhi silaha zilizotumika kipindi cha uhuru, kuna vijana watatu waliingia ndani hatujui walikwenda kufanya nini lakini ghafla mlipuko ulitokea na hakuna hata mmoja aliyetoka, hivyo ilikuwa ni ajali,” alisema.
Aliongeza kuwa tathmini ilifanyika na waathirika walilipwa fidia zao kama walivyostahili lakini baada ya muda baadhi yao walianza kulalamika kuwa fedha walizopewa hazikutosha.
“Hali hii ilitoa funzo kwetu katika mlipuko wa Gongo la Mboto, waathirika hawakulipwa fedha taslimu bali walijengewa nyumba na kila mmoja alikabidhiwa funguo, hatua iliyosaidia kuepuka migogoro kama iliyotokea Mbagala,” alisema Kikwete.
Aliongeza:” Naamini hata leo ikitokea rais ametembelea eneo hilo kuna watu watalalamika kuwa hawakulipwa fidia au walipewa kidogo ilihali walilipwa lakini hawakuzitumia fedha hizo kwa matumizi yaliyokusudiwa ikiwemo ujenzi wa nyumba zao”.
Kuhusu sera ya uchumi wa buluu, Kikwete alisema ni mkakati wa kutumia bahari kama rasilimali ya kukuza uchumi kupitia uvuvi wa samaki, matumizi ya bandari kwa kupokea na kusafirisha bidhaa, pamoja na kuendeleza sekta ya utalii.
