DODOMA: WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Prof. Riziki Shemdoe ameridhishwa na maandalizi ya mapokezi ya wanafunzi wa darasa la awali na la kwanza katika Shule ya Msingi Iyumbu jijini Dodoma.
Amesema kuwa maandalizi katika shule zote za msingi 18055 yamekamilika na zipo tayari kupokea wanafunzi kuanzia Januari 13, 2026.
Prof Shemdoe ameitembelea shule hiyo leo Januari 12, 2026, kujionea maandalizi ya mapokezi ya wanafunzi wanaotarajiwa kuanza darasa la awali na la kwanza.
“Tumeona maandalizi kwenye shule hii yamekamilika, kama ilivyo kwenye shule zote 18055 za msingi, hivyo natoa wito kwa wazazi wenye watoto walio na umri wa kuanza darasa la awali na la kwanza wawapeleke shuleni,” Prof. Shemdoe amesisitiza.
Prof. Shemdoe amejionea madarasa ya awali ambayo yamejengwa kwa fedha za mapato ya ndani ya Halmashauri ya Jiji la Dodoma, na kuzielekeza halmashauri zote nchini kutumia mapato ya ndani kujenga miundombinu bora ya elimu kama ambavyo Halmashauri ya Jiji la Dodoma imejenga katika Shule ya Msingi Iyumbu.
Aidha, Prof. Shemdoe amewataka walimu nchini kuhakikisha shule zinatoa wanafunzi wenye ufaulu mzuri kwani Rais Dk. Samia Suluhu Hassan amekuwa akitoa fedha nyingi kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu ya elimu, hivyo ufaulu wa wanafunzi ni faraja kwa Rais.

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule amesema kwamba tangu Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan aingie madarakani ufaulu umeongezeka, na kuongeza kuwa sababu kubwa ya kuongezeka kwa ufaulu huo ni uwekezaji fedha nyingi katika ujenzi wa miundombinu ya elimu.
Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Iyumbu, Monica Nshimba amemshukuru Prof. Shemdoe kwa kuitembelea shule yake na kumuahidi kwamba walimu wako tayari kufanya kazi kwa bidii na weledi ili kutimiza lengo la Serikali la kutoa elimu bora ya msingi kwa wananchi wake.
Naye, Diwani wa Kata ya Iyumbu Sadiki Mponyamili amemshukuru Mhe. Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kwa kuipatia kata yake fedha nyingi kwa ajili ya kuboresha Shule ya Msingi Iyumbu na ameipatia kata yake zaidi ya Sh Milioni 150 kwa ajili ya kuboresha shule ya sekondari.
