Serikali ya Somalia ilitangaza kufutilia mbai mikataba yote na UAE inayojumuisha ile ya bandari na ushirikiano wa ulinzi na usalama na ikitoa ushahidi kwamba Umoja huo wa Falme za Kiarabu umeyahujumu mamlaka ya taifa hilo la Pembe ya Afrika.
Katika taarifa yake, waziri wa habari wa Somalia Daud Aweis Aden Duale, alithibitisha kuchukuliwa kwa hatua hiyo.
” Baada ya kutathmini kwa makini matukio ya hivi punde na kutumia mamlaka yake ya kikatiba, Baraza la Mawaziri linafutilia mbali na kubatilisha makubaliano yote yaliyopo na serikali ya Umoja wa Falme za Kiarabu, ikiwa ni pamoja na yale yanayohusisha taasisi za utawala za serikali, na majimbo ya shirikisho ndani ya Jamhuri ya Shirikisho la Somalia. Uamuzi huu unahusu makubaliano yote na mipangilio ya uendeshaji wa bandari za Berbera, Bosaso na Kismayo.”
Taarifa hiyo haikutaja moja kwa moja kutambuliwa kwa Somaliland au madai ya Saudi Arabia ya wiki iliyopita kwamba UAE ilimsaidia , Aidarous Al-Zubaidi, kutoroka kwa boti na ndege kupitia Berbera na mji mkuu wa Somalia, Mogadishu,hadi Abu Dhabi .
Shirika la uhamiaji la Somalia limesema linachunguza madai ya matumizi ambayo hayakuidhinishwa ya anga la Somalia pamoja na viwanja vyake vya ndege.
Afisa mmoja mkuu katika ikulu ya rais wa Somalia, ameliambia shirika la habari la AFP kwa sharti la kutotajwa jina kuwa uamuzi huo ulitokana na ripoti za kuaminika na ushahidi wa kutosha kuhusu vitendo vya uhasama vinavyohujumu mamlaka ya dola, umoja wa taifa, na uhuru wa kisiasa wa nchi.
Hata hivyo hakukuwa na tamko la haraka kutoka kwa mamlaka za UAE.
Tofauti zilizoko kati ya Somalia na UAE
Kumekuwa na tofauti kubwa kati ya Somalia na UAE kuhusu masuala kadhaa. Umoja wa Falme za Kiarabu unaonekana kuunga mkono kimya kimya hatua ya Israel mwezi uliopita ya kuitambua Somaliland, ikiwa nchi ya kwanza kufanya hivyo tangu eneo hilo kujitangazia uhuru wake kutoka kwa Somalia mwaka 1991.
UAE ilijenga na inaendesha bandari kubwa na kambi ya kijeshi katika eneo la Berbera huko Somaliland.
Katika taarifa yake hiyo ya jana, serikali ya Somalia ilisema UAE haitaruhusiwa tena kufanya shughuli zake huko Berbera, ingawa Mogadishu ina mamlaka ya kinadharia tu katika jimbo hilo lililojitenga na Somalia kwa takribani miongo mitatu sasa.
