SERIKALI ya Tanzania imeweka malengo makubwa kuhakikisha inafufua viwanda mkoani Tanga ili kuongeza fursa za ajira kwa wananchi na kuongeza wigo wa mapa- to ya serikali.
Hii inakwenda sambamba na utekelezaji wa Dira ya Maendeleo ya Taifa ya Mwaka 2025 inayolenga kuipeleka Tanzania kwenye uchumi wa viwanda na kuongeza wigo wa uzalishaji wa bidhaa za ndani ili kulinda viwanda vya ndani.
Kimsingi, Rais Samia Suluhu hassan ameonesha dhamira ya kurejesha Tanga ya viwanda na ili kufikia dhamira hiyo, tayari serikali kupitia Wizara ya Viwanda na Biashara imeshaanza kulifanyia kazi suala hilo. Hivi karibuni Waziri wa Viwanda na Biashara,
Judith Kapinga alifanya ziara mkoani Tanga kutembelea baadhi ya viwanda vilivyoanza kufufuliwa. Katika ziara hiyo, Judith anasema serikali imeanza kuona matokeo chanya ya utekelezaji wa maelekezo ya Rais Samia.
Anasema katika kipindi cha takribani miezi tisa hadi kumi hivi, wizara kwa kushirikiana na serikali ya mkoa imetekeleza kwa vitendo maelekezo ya Rais Samia ya ufufuaji wa viwanda 18 katika hatua ya awali.
SOMA: Agizo la Tanga ya viwanda laanza kutekelezwa
Miongoni mwa viwanda hivyo, vipo vilivyokuwa vimebinafsishwa na serikali na ambavyo vipo chini ya watu binafsi. Viwanda vilivyofufuliwa hadi sasa ni pamoja na Kiwanda cha Unique Steel Rolling kinachozalisha bidhaa za chuma,
Kiwanda cha Ply and Panel kinachotengeneza bidhaa za mbao pamoja na Kiwanda cha African Harmony kinachozalisha bidhaa za sabuni. Tayari viwanda hivyo vimeanza uzalishaji. Amesema ili kufikia ufufuaji wa viwanda, walifanya majadiliano na wawekezaji yaliyozingatia changamoto za jumla na za binafsi zinazokikabili kila kiwanda ili kuweka mikakati madhubuti ya urejeshwaji.
“Kwa kushirikiana na serikali ya mkoa, naomba tukiri kwamba jitihada hizo zimeweza kuzaa matunda kwani tayari vimeshaanza uzalishaji na leo nimekuja maalumu kujionea kama wameweza kutimiza ahadi yao,” anasema Judith katika ziara hiyo.
Anatoa mfano wa Kiwanda cha African Hamon ambacho kilikuwa hakifanyi kazi kabisa lakini sasa kimeanza kufanya kazi. Kiwanda hicho tayari kimeajiri zaidi ya vijana 200 kwa ajira za kudumu, jambo linalosaidia kuongeza ajira miongoni mwa vijana mkoani Tanga.
Kwa upande wa Kiwanda cha Unique Steel Rolling kinachozalisha bidhaa za Chuma, Judith anasema tayari mwekezaji ameanza majaribio ya uzalishaji. Anatarajia kuzalisha tani 30 hadi 40 katika kipindi cha miezi mitatu.
Vilevile katika Kiwanda cha Ply and Panel kinachozalisha bidhaa za mbao, Judith anasema kimefanyiwa
ukarabati mkubwa ikiwa ni pamoja na uwekaji wa mashine mpya sambamba na ukarabati wa jengo uliohusisha uwekaji wa paa ambalo awali halikuwapo.
“Mwekezaji katika kiwanda hicho ameweza kufunga mashine mpya nne huku ukarabati ukiwa umeweza kufikia asilimia 60 na ametuhakikisha kuwa hivi karibuni ataweza kuanza uzalishaji wa bidhaa kwa majaribio,” anasema.
Kwa mujibu wa Judith, lengo la serikali kupitia wizara hiyo ni kuhakikisha viwanda vyote vinavyolengwa vinaanza kufanya kazi kikamilifu ili kuimarisha soko la ndani na nje ya nchi kupitia bidhaa zinazozalishwa nchini.
Ili kuhakikisha mambo yanakwenda vyema, serikali itaweka mwakilishi katika kila kiwanda ili kurahisisha utatuzi wa changamoto za wawekezaji na kuhakikisha kipaumbele kinatolewa kwa haraka.
Katika ziara hiyo, Judith anasema juhudi hizo zinaendana na maono ya Rais Samia ya kuifanya Tanzania kuwa nchi ya viwanda huku viwanda hivyo vikichangia moja kwa moja kuboresha maisha ya wananchi kupitia ajira za uhakika.
Mpango huo umeelezwa wazi katika Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya mwaka 2025–2030 na Dira ya Maendeleo ya Taifa ya mwaka 2050 inayolenga kukuza uchumi wa viwanda na maendeleo endelevu. Waziri huyo anabainisha kuwa, malengo yaliyopo ni kuhakikisha viwanda 18 vya awali vinarudi katika uzalishaji wa bidhaa na khakiki- sha bidhaa zinazozalishwa zinaingia sokoni ili kuimarisha pato la nchi.
“Kama wizara, kazi yetu kubwa ni kuwapa ushirikiano wawekezaji kwa kuwahakikishia mazingira rafiki ya uwekezaji wao sambamba na na kushughulikia haraka changamoto zao,” anasema.
Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Dk Batilda Burian anasema kuanza kwa uzalishaji wa viwanda hivyo ni sehemu ya mchango mkubwa kwa wizara na serikali ya mkoa kuhakikisha dhamira ya ‘Tanga ya Viwanda’ inaleta matokeo tarajiwa kwa wananchi na nchi kwa ujumla.
“Tanga ya Viwanda ni kilio cha muda mrefu cha mkoa huu ambao ulikuwa ni wa pili nchini kwa kuwa na viwanda vingi lakini vikabaki kama magofu, sasa watu wa tanga wanafurahi kuona viwanda vikifufuliwa,” anasema Dk Batilda.
Anaongeza kuwa, serikali mkoani Tanga imejipanga kufanya ufuatiliaji wa kufufua viwanda hivyo vya awali kwa kuhakikisha vinafufuliwa na kufanya kazi ili kuongeza wigo wa ajira kwa wananchi mkoani humo. Aidha, anasema serikali inasisitiza kuhakikisha Tanga inakuwa mkoa wa viwanda.
Anaomba serikali kuongeza gati ya pili bandarini ili kurahisisha huduma kwa kuwezesha meli nyingi kutia nanga bandarini. Dk Batilda anadokeza kuwa, wanatarajia kufanya mkutano mkubwa wa kunadi fursa zilizopo mkoani Tanga.
Kwa mujibu wa mkuu wa mkoa huyo, tayari Mkoa wa Tanga una sera ya kuwa na viwanda vipya katika kila wilaya kuanzia vikubwa, vya kati hadi vidogo ili kuongeza uzalishaji wa bidhaa na kufungua fursa za ajira kwa wananchi.
“Tunaweka msisitizo mkubwa ili viwanda vipya vinavyokuja na vya zamani viweze kuendelea kufanya kazi kubwa ili picha ya Tanga ya Viwanda iweze kurejea na kuonekana katika uhalisia wake,” anasema Dk Batilda. Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo la Tanga Mjini, Kassimu Mbaraka anasema wananchi wa Tanga watanufaika na fursa lukuki kutokana na kuwapo kwa viwanda hivyo.
Mbaraka anahimiza wananchi kuchangamkia fursa hizo na wamiliki wa viwanda ambavyo havijafufuliwa kushirikiana na mamlaka husika kuhakikisha viwanda vyote vinafanya kazi na kuwanufaisha wao, jamii na taifa kwa ujumla.
“Wito wangu kwa wananchi wa Tanga kuchangamkia fursa ya Tanga ya Viwanda kwa kupata ajira lakini pia na bidhaa zinazozalisha kuzitumia kuuza ili kuimari- sha vipato vyetu na kukuza uchumi wetu,” anasema mbunge huyo. Wafanyakazi wa Kiwanda cha Steel and Rooling wakimwonesha Waziri wa Viwanda na Biashara, Judith Kapinga na viongozi wengine wa Mkoa wa Tanga nondo zinazozalishwa kiwandani hapo.
Serikali ya Awamu ya Nane Zanzibar inayoongozwa na Rais, Dk Hussein Mwinyi imeweka nguvu kubwa kuboresha sekta ya elimu. Waziri Mkuu, Dk Mwigulu Nchemba akifungua Shule ya Sekondari Chukwani, Zanzibar hivi karibuni.
