DAR ES SALAAM: Tathmini ya data za mitetemo za 3D zilizochukuliwa katika Kitalu cha Utafutaji wa Mafuta na Gesi Asilia cha Ruvuma kilichopo mkoani Mtwara imeonesha uwezekano wa uwepo wa futi za Ujazo trilioni 3.45 za gesi asilia tofauti na Futi za Ujazo Trilioni 1.87 zilizoripotiwa awali.
Meneja mkuu wa kampuni ya ARA Petroluem Tanzania Ltd (APTL) inayoendesha kitalu cha Ruvuma Erhan Saygi amebainisha hayo leo, Januari 13, 2026, jijini Dar es Salaam katika warsha iliyoandaliwa na Kampuni hiyo kwa lengo la kueleza namna tathmini iliyofanyika imeongeza uelewa wa jiolojia ya Kitalu cha Ruvuma na kuamsha matumaini ya uwezekano wa ugunduzi zaidi wa gesi asilia katika Kitalu hicho.
Akizungumza katika warsha hiyo, amesema kuwa kazi kubwa iliyofanyika ya kuchakata na kutathmini taarifa za mitetemo iliyokusanywa kupitia teknolojia ya 3D katika eneo lenye jumla ya kilomita za mraba 338 zilizochukuliwa mwaka 2022 iliwezesha kampuni hiyo kuwa na uelewa mpana wa Kitalu cha Ruvuma.
“Matokeo ya tathmini ya data za mitetemo za 3D zilizochukuliwa na kuchakatwa pamoja na tathmini ya data nyingine zilizokuwepo katika Kitalu cha Ruvuma zikiwemo data za mitetemo za 2D na data za visima vilivyochimbwa katika Kitalu hicho kumeipa APTL matumaini ya kugundua gesi asilia zaidi katika Kitalu hiki” alisema Erhan.
Kupitia warsha hiyo iliyohudhuriwa na wawakilishi kutoka Mamlaka ya Udhibiti Mkondo wa Juu wa Petroli (PURA) na Shirika la Maendeleo ya Petroli (TPDC), kampuni ya APTL ilisema kufuatia matumaini hayo, kampuni hiyo itaendelea kufanya tafiti zaidi katika eneo la Ntorya ili kuhakikisha uwepo wa kiasi hicho cha gesi asilia.
Kwa mwaka 2026, APTL na wabia wake katika Kitalu cha Ruvuma (TPDC na Kampuni ya Ndovu Resources Ltd) watafanya ukarabati wa kisima cha Ntorya 1 na majaribio ya kisima cha Ntorya 2. Visima vyote viwili vitakuwa visima vya uzalishaji. Aidha, kampuni hiyo na wabia wake watachimba kisima cha uhakiki cha Chikumbi 1.
