DAR ES SALAAM: Chama cha Wahasibu Tanzania (NBAA) kimeandaa Siku ya Kazi kwa Wahasibu (Annual Accountancy Career Day) jijini Dar es Salaam, kwa lengo la kuwakutanisha wanafunzi wa fani ya uhasibu, wahitimu, waajiri pamoja na wahasibu wabobezi ili kujadili kwa pamoja mustakabali wa taaluma hiyo.
Mwenyekiti wa Bodi ya NBAA, Silvia Temu, amesema wazo la kuanzisha ‘Career Day’ lilitokana na haja ya kuwa na siku maalum ya kuwakutanisha wanafunzi, CPA candidates na waajiri ili waweze kuzungumza ana kwa ana kwa mara ya kwanza katika mfumo rasmi.
“Tulikuwa tunatafuta siku ya kukutanisha wanafunzi, candidates na waajiri tuzungumze kwa pamoja. Hii ni fursa ya kipekee inayokutanisha kizazi kipya cha wahasibu na wahasibu wabobezi pamoja na waajiri kutoka taasisi za binafsi na za serikali,” amesema Temu.
Ameeleza kuwa lengo kubwa la tukio hilo ni kuwasaidia wanafunzi na wahitimu kuunda maono sahihi kuhusu taaluma ya uhasibu, kujua matarajio ya soko la ajira na changamoto zilizopo katika fani hiyo.
“Tunawataka washiriki wazungumze kuhusu mwanzo wao na changamoto zao katika taaluma. Ni nafasi ya kupima kama yale wanayojifunza darasani yanaendana na mahitaji ya soko la ajira, lakini pia ni fursa ya kupata ajira au mentorship kutoka kwa waliopo tayari kwenye fani hii,” amesema.

Katika tukio hilo, NBAA pia ilizindua rasmi jukwaa la kidijitali lijulikanalo kama NBAA Accountancy Hub, litakalotumika kuwaunganisha wanachama, wanafunzi na wahasibu kwa kutoa taarifa mbalimbali za kitaaluma ikiwemo mabadiliko ya kisheria na taarifa muhimu za fani.
“Hub hii ni chombo kitakachotuunganisha na kutusaidia kukuza taaluma yetu kwa kutoa taarifa za kitaaluma kwa wakati,” amesema Temu.
Akizungumza kwa niaba ya uongozi wa CPS, Mkurugenzi Puis Maneno amesema mpango huo ni nguzo muhimu katika kuwaandaa wanafunzi wa CPA kwa maisha ya kazi kwa vitendo, kwa kuwaunganisha kati ya darasa na mazingira halisi ya kazi.
“Ni daraja kati ya elimu ya darasani na dunia ya kazi. Uhasibu ni lugha ya biashara, na tukio hili litawaongoza washiriki kuelekea mafanikio ya taaluma zao,” amesema Maneno.
Ameongeza kuwa katika Career Day hiyo, kuna mabanda zaidi ya 20 ya waajiri kutoka taasisi mbalimbali ikiwemo benki, mashirika ya umma na sekta binafsi, ambao wanazungumza moja kwa moja na washiriki kuhusu fursa za ajira, mafunzo kwa vitendo na mentorship.
Baadhi ya washiriki wameeleza kufurahishwa na tukio hilo. Lucy Pima, mwanafunzi wa mwaka wa mwisho wa Shahada ya Uhasibu na Kodi (Accounting and Taxation) katika Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE), amesema amehudhuria ili kujifunza zaidi kuhusu taaluma yake na kuanza kujenga mtandao wa kitaaluma.

“Niko mwaka wa mwisho, nikimaliza mwaka huu natakiwa kujiunga na CPA. Nimekuja kujifunza zaidi, kukutana na waajiri na kupata mawasiliano. Natamani kukutana na Bi Silvia Temu ili anipe ushauri au kunimentor, namuona kama kielelezo kinachonihamasisha kusoma kwa bidii,” amesema.
Naye Halima Kassim, mwanafunzi wa CBE anayesoma Uhasibu na Kodi, amesema lengo lake ni kufahamu zaidi NBAA na kuelewa mahitaji ya soko la ajira.
“Nimekuja kujua NBAA ni nini, kujua tunapokosea kama wanafunzi na soko linahitaji nini. Pia ni nafasi ya kufanya networking na kuona kama Accountancy Hub itatusaidia kupata taarifa mbalimbali,” amesema.
Hata hivyo, Halima ameshauri tukio hilo lifanyike zaidi ya mara moja kwa mwaka na vyuo vipatiwe fursa kwa awamu.
“Washiriki ni wengi sana, wengine wanakosa nafasi ya kushiriki kikamilifu. Ni vizuri lifanyike zaidi ya mara moja kwa mwaka au wachukue vyuo viwili au vitatu kwa awamu,” amesema.
Kwa ujumla, Career Day ya NBAA imeonekana kuwa jukwaa muhimu la kuwaunganisha wanafunzi, wahitimu, waajiri na wahasibu wabobezi, na kuweka msingi wa kukuza taaluma ya uhasibu nchini kupitia mawasiliano ya moja kwa moja na matumizi ya teknolojia ya kidijitali.
