
Wiki mbili tayari zimepita nchini Cameroon tangu Paul Biya, katika hotuba yake ya Mwaka Mpya, alipotangaza “serikali mpya” itakayoundwa “katika siku zijazo.” Ingawa “siku zijazo” ziko wazi kwa tafsiri, hii ni mara ya kwanza Paul Biya mwenyewe kutangaza mabadiliko ya baraza la mawaziri, licha ya kufanya zaidi ya miaka thelathini madarakani katika historia yake.
Imechapishwa:
Dakika 2 Wakati wa kusoma
Matangazo ya kibiashara
Serikali ya sasa, inayoongozwa na Waziri Mkuu Joseph Dion Ngute, imekuwapo kwa miaka saba bila uteuzi mpya, licha ya vifo na kujiuzulu kwa mawaziri, wakiwemo Bello Bouba Maïgari na Issa Tchiroma Bakary, wagombea katika uchaguzi wa urais wa mwezi Oktoba mwaka uliyopita, na kashfa kadhaa, haswa za kifedha.
Kulingana na Christophe Mien Zock, mkurugenzi wa propaganda katika chama cha CPDM: “Uchaguzi huu wa urais ulionyesha wazi kwamba raia wa Cameroon hawakuridhika na utawala na baadhi ya maendeleo ya miundombinu.”
Anabaini kwamba katika hotuba yake, Paul Biya alielezea wasifu wa timu ya baadaye. “Uadilifu. Kwetu sisi, hii ina maana kwamba rais anafahamu kwamba wakati mwingine tumepotoka kutoka kwa mawazo haya ya mabadiliko. (…) Na kwa hivyo tangazo hili linaweza tu kuwapa wanachama wa chama imani fulani. Lakini, kama wanavyosema, tunasubiri kuona jinsi mambo yatakavyokuwa.”
Katika Chama cha PCRN cha Cabral Libii, ambaye alishika nafasi ya tatu katika uchaguzi wa urais, wanasema wanazingatia uchaguzi wa wabunge na manispaa, lakini wako tayari ikiwa wataitwa, kama ilivyoelezwa na msemaji wa chama hicho Richard Tamfu.
“Sijui kama, katika maono yake, anakusudia kuunda serikali jumuishi, lakini sisi katika PCRN tuanona kwamba hatuwezi tukatengwa. (…) ikiwa, kwa bahati, tungeitwa kuwatumikia watu wa Cameroon, tuko tayari.”
Kwa Hermine Patricia Tomaïno Ndam Njoya, mwanachama wa upinzani wa Chama cha UDC, hata hivyo, hakuna cha kutarajia kutokana na mabadiliko hayo. “Hapana, haitakuwa mabadiliko ya kweli, kwa kuwa tuna uzoefu tangu mwaka 1991. Kuna watu wanaorudi, lakini miradi yao inazuiwa na ajenda ya utawala unaokataa kushiriki katika umoja wa kitaifa.” Kwake, ni umoja wa kweli wa kitaifa pekee, wenye maoni inayojumuisha mabadiliko ya katiba na kanuni za uchaguzi, unaoweza kuiondoa Cameroon katika mkwamo huu.
Katika chama cha MRC cha Maurice Kamto, hawako tayari hata kutoa maoni, wakipinga uhalali wa muhula wa nane wa Paul Biya.
