Makonda aanza kazi, ataka watendaji wizara wajipimeMakonda aanza kazi, ataka watendaji wizara wajipime

WAZIRI wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Paul Makonda (Pichani) amekabidhiwa rasmi ofisi na aliyekuwa Waziri wa wizara hiyo, Profesa Palamagamba Kabudi na kutaka watendaji wote wa wizara hiyo kuhakikisha wanakaa kwenye viti vyao na kuenea.

Alieleza hayo jijini Dodoma baada ya kuapishwa na kueleza kuwa hana tabia ya kumchekea mtu wakati moyoni mwake amechukia au kumnunia wakati anamfurahia na kwamba wataiona furaha yake na hasira pia.

“Naomba watendaji kila mtu ukae kwenye kiti chako uenee na ufunge mkanda wako vizuri,” alisema Makonda.

Alieleza sifa yake mojawapo ni kuwa na kasi ya utekelezaji wa majukumu na hana muda wa kusubiri jambo lifanyike na kuwataka watendaji hao kwenda na kasi hiyo.

“Mimi muda wa kusubiri sina, umri wangu nisipokuwa na spidi ya kutimiza ndoto za Watanzania waliomwamini Samia (Rais Samia Suluhu Hassan) wakamteua na mimi nitakuwa siandiki alama njema kwenye kizazi chetu,” alieleza.

Alisema pamoja na Profesa Kabudi kubadilishiwa majukumu, atabaki kuwa mlezi wa wizara hiyo na kwamba kila alichotamani kitokee kitatokea.

“Kila nilikopita nimeweka alama ya kutokubeza watangulizi wangu, kulinda na kuendeleza kazi walizofanya ili kwa pamoja tuwe na historia njema kama taifa ya kuwa na mwendelezo wa watumishi,” alifafanua.

Makonda alisema kwa kuwa vijana wengi wamejiajiri kwenye habari hasa televisheni za mtandaoni na mitandao ya kijamii, atamuomba Rais Samia awapatie Sh bilioni moja au mbili ili kuwakopesha vijana hao wawe na vifaa vyao wenyewe na waweze kutengeneza maudhui ambayo dunia itaziona na kuiona Tanzania katika taswira nzuri.

Pia, alisema wanaendelea na majadiliano ili wizara hiyo iwe na kitengo cha mawasiliano ya lugha mbalimbali za kimataifa ili yanapotokea matukio ya kimataifa yafikie vyombo vya kimataifa na hatimaye kuimarisha taswira ya nchi.

“Tutaweka timu ambayo kazi yake ni habari ikifanyika inachukuliwa inapelekwa kwenye vyombo vya kimataifa ili sura yetu na mwonekano wetu uendelee kuimarika kule,” alifafanua.

Kwa upande wake, Profesa Kabudi alisema anaridhika kuondoka wizarani hapo huku mambo mengi aliyohimiza yafanyike yakiwa yamefanyika na kuwakumbusha idara na vitengo vyote kukabidhi utekelezaji wa maagizo 49 waliyopewa katika siku 3 za kikaokazi kilichofanyika, mwaka jana Kibaha mkoani Pwani.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *