SHINYANGA: WALIMU wa Shule ya Msingi Halmashauri ya Msalala wilayani Kahama mkoani Shinyanga    wametakiwa kufuata waraka wa elimu wa mwaka 2016 kuwa elimu ni bure nawasitoze fedha zozote kwa wazazi wanapokwenda kuwaandikisha watoto darasa la awali na  darasa kwanza.

Ofisa elimu msingi kutoka halmashauri hiyo, Kaseku Sheja amesema hayo mbele ya Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Mboni Mhita kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika kata ya Segese baada ya kusikiliza kero kutoka kwa baadhi ya wazazi.

Sheja amesema elimu ni bure na wazazi wanatakiwa kununua sare za shule na michango ya chakula na mingine itakayojitokeza kwenye shule husika hayo ni makubaliano ya kwenye vikao vya shule na wazazi sio ya kwenye waraka wa elimu ambao unaeleza wazi.

“Utozwaji fedha ni ridhaa kati ya wazazi na walimu zipo shule zilizofikia hatua ya wazazi kupika chakula wenyewe shuleni bila kulazimishwa  lengo watoto wao wapate chakula na watoto kukaa bila chakula shuleni huko nikuwatesa,”amesema Sheja.

Sheja amewataka walimu wakuu wa shule  watoe maelekezo ya namna shule zifuate za utozaji fedha na sio kumlazimisha mzazi hata akiwa hana sare mtoto aandikishwe ili mzazi akaangalie utaratibu wa kumnunulia.

Sheja amesema serikali inatoa mshahara sio sadaka inataka walimu wafanye kazi na wale wenye kazi zingine pembeni wasiache vipindi nakuleta uzembe wa kutofundisha kwani hatua kali itachukuliwa.

Mboni Mhita amesema utozwaji wa fedha kwa ajili ya kumuandikisha mtoto hilo halikubaliki kwani elimu ni bure kuanzia msingi hadi sekondari  na utozwaji wa masuala mengine labda yafanyike makubaliano ya pande zote walimu na wazazi.

“Isitokee mwalimu anatamka mtoto asije shuleni sababu hana hela ya kitu fulani tutamchukulia hatua aende akasome waraka vizuri,” amesema Mhita.

Mzazi Rajabu Charles mkazi kutoka kijiji cha Segese amesema kero kubwa aliyonayo ni mtoto wake alipokwenda kumuandikisha darasa la kwanza walimu walimtoza fedha na kilo za mchele ili aandikishwe lakini alishindwa kutokana na kukosa fedha.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *