Chanzo cha picha, AFP via Getty Images
Rais wa Marekani, Donald Trump, ametoa ujumbe usiotarajiwa kwa wananchi wa Iran wanaoendelea kuandamana dhidi ya serikali katika miji kadhaa kwa zaidi ya wiki mbili sasa.
Kupitia mtandao wake wa Truth Social siku ya Jumanne, Trump aliwahimiza waandamanaji hao kuendeleza shinikizo lao dhidi ya mamlaka.
“Wazalendo wa Iran, endeleeni kuandamana. Dhibitini taasisi zenu. Andikeni majina ya wauaji na wahusika wa ukiukwaji wa haki za binadamu. Watalipa gharama kubwa,” aliandika.
Trump pia alitangaza kusitisha mawasiliano ya kidiplomasia na Tehran, akisema: “Nimefuta mikutano yote na maafisa wa Iran hadi mauaji yasiyo na maana dhidi ya waandamanaji yakomeshwe. Msaada uko njiani.”
Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Wanaharakati wa Haki za Binadamu (HRANA) lenye makao yake Marekani, zaidi ya watu 2,500 wamepoteza maisha tangu maandamano hayo yalipoanza tarehe 28 Desemba.
Takwimu hizo zinafanana na kauli ya afisa mmoja wa Iran aliyekiri kuwa takribani watu 2,000 wameuawa ikiwa ni mara ya kwanza kwa utawala wa Aayatola kukubali hadharani ukubwa wa vifo vinavyohusishwa na maandamano hayo, ingawa uliwalaumu wahusika wa nje kwa machafuko hayo.
Alipoulizwa kuhusu taarifa kwamba baadhi ya waandamanaji walikuwa wanakabiliwa na adhabu ya kifo Jumatano, Trump alisema Marekani ingechukua “hatua kali sana” iwapo mauaji hayo yangetekelezwa.
Kwa upande wake, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Abbas Araghchi, alijibu kwa kuonya kuwa taifa lake litajilinda dhidi ya “uovu wa kigeni na kuingiliwa kwa masuala yake ya ndani.”
Kauli hiyo ilionekana kuashiria kuongezeka kwa mvutano kati ya mataifa hayo mawili.
Chapisho la Trump lililosisitiza maneno “MSAADA UKO NJIANI” lilitafsiriwa na wachambuzi kama ishara wazi ya nia ya Marekani kuingilia kati kwa njia ya moja kwa moja.
Wakati huo huo, maafisa wakuu wa serikali ya Marekani wanatarajiwa kukutana Ikulu ya White House Jumanne hii kujadili hatua mbadala zinazoweza kuchukuliwa.
Ingawa mwishoni mwa wiki Trump alikuwa ameashiria uwezekano wa kufungua njia za kidiplomasia kufuatia madai ya pendekezo la mazungumzo kutoka Iran, inaonekana juhudi hizo zimesitishwa kwa sasa.
Kwa mtindo wake unaotambulika wa kutumia lugha kali mtandaoni, Trump mara nyingi hutumia herufi kubwa kusisitiza vitisho au maonyo, ingawa si mara zote hutekeleza aliyoyasema.
Hata hivyo, kwa kuzingatia ukubwa wa vifo vilivyoripotiwa na ahadi yake ya wazi ya kuwaunga mkono waandamanaji wa Iran, inaonekana Rais wa Marekani tayari amechukua mwelekeo thabiti.
”Kwa hali ilivyo sasa, ni vigumu kuona akirudi nyuma”,mchambuzi wa masuala ya kisiasa Iran anaeleza.
Soma Zaidi: