ARUSHA: Ubora, mshikamano na kiu ya ushindi ndivyo vilivyoibeba timu ya Ulipo Tupo Lake Zone mpaka kutwaa ubingwa wa soka wa CRDB Super Cup msimu wa tano, baada ya kuifunga timu ya CRDB Wakala Central Zone goli 1_0 katika mchezo wa fainali wenye ushindani mkubwa uliochezwa katika uwanja wa Shekh Amri Abeid Jijini Arusha.

Kwa Matokeo hayo timu Ulipo Tupo ilifanikiwa kupata zawadi ya kitita cha fedha taslimu Sh milioni 15 na kikombe ambapo kwa upande wa mpira wa pete, mvutano ulikuwa mkubwa kati ya timu vya Ulipo Tupo Queens na timu ya Popote Inatiki Queens, ambapo Ulipo Tupo Queens Central Zone iliibuka mshindi wa magoli 40 kwa 30 na kujinyakulia zawadi ya Sh milioni 11 fedha taslimu.

Akizungumza baada ya fainali hiyo, Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Amosi Makallah, amesema mashindano hayo yamekuwa chachu ya kukuza uchumi wa Mkoa huo na sehemu ya maandalizi ya AFCON 2027.
Makallah alisema mbali ya hilo Mashindano ya CRDB ni miongoni mwa mashindano bora nchini Tanzania yenye kujenga afya na kukimbiza magonjwa nyemelezi hivyo taasisi zingine zinapaswa kuiga.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela, amesema benki hiyo itaendelea kuwekeza kwenye michezo kwa maendeleo ya jamii.
Nsekela alisema mashindano hayo hufanyika kila mwaka na msimu huu wa tano uliofanyika jiji Arusha unalenga kuhimiza michezo kazini na kujenga afya ili kuondokana na magonjwa nyemelezi ambayo kufanya mazoezi ni moja ya kinga kubwa.

Naye Hashimu Makinda kepten wa timu ya Ulipo Tupo alisema kuwa ushindi wa kutwa kombe la ubingwa ni kutokana na maandalizi mazuri ya wachezaji na kujituma na kusema hakuna njia ya mkato katika mafanikio katika soka bila kuwa na maandalizi bora.
