Tangu mwishoni mwa wiki iliyopita, video kadhaa zimekuwa zikisambaa kwenye mitandao ya kijamii nchini Ukraine zikionyesha watu binafsi wakiwasilishwa kama wapiganaji wa Kiafrika katika jeshi la Urusi. Video hizo zinaonyesha wanaume wakidhalilishwa au kutendewa kama wanyama. Ingawa video hizo bado hazijathibitishwa rasmi, zinaonekana kuaminika kwa wataalamu waliohojiwa na RFI.

Imechapishwa:

Dakika 1 Wakati wa kusoma

Matangazo ya kibiashara

Chunguzi kadhaa wa waandishi wa habari na ripoti za wataalamu zimeonyesha kuwa raia wengi wa Kiafrika, waathiriwa wa mipango ya ajira za uongo, huishia kutumwa kwenye mstari wa mbele.

Katika video ya kwanza, mtu mmoja anasema jina lake ni Francis. Anaonekana kuwa na uoga usoni mwake. Bomu limefungwa kifuani mwake. Mtu anayepiga picha anamtukana, anamtishia, na kumwamuru akimbie “kufungua lango.” Video ya pili imerekodiwa katika msitu wenye theluji. Kundi la watu hao linaimba wimbo wa kijeshi wa Uganda. Mtu anayepiga picha anawataja kama “watu wa kutupwa.”

Thierry Vircoulon, mtafiti msaidizi katika Taasisi ya Mahusiano ya Kimataifa ya Ufaransa na mwandishi wa ripoti kuhusu sera ya  Urusi ya kuajiria watu kutoka barani Afrika, anachambua video hizi. “Wakati wa utafiti wetu, tuliangazia ukweli kwamba mara nyingi waliwekwa katika vitengo vilivyotumwa kwenye mstari wa mbele katika maeneo hatari zaidi, mara nyingi ili kugundua ngome za wanajeshi wa Ukraine. Na kwa hivyo, bila shaka hii ndiyo maana ya maoni kuhusu kuwa watu wa kutupwa, kwani kiwango cha vifo ni kikubwa katika vitengo hivi kwa sababu vinashiriki katika shughuli hatari zaidi.”

Video zingine zinaonyesha watu weusi wakivaa sare za kijeshi wakilengwa na ndege zisizo na rubani au kuomba kurejeshwa katika nchi zao za asili, pamoja na mahojiano na wafungwa. Zikirushwa kwenye mitandao ya kijamii nchini Ukraine, video hizi zinatimiza madhumuni mawili, kulingana na Thierry Vircoulon. “Lengo ni kufichua kwamba kuna mamluki katika jeshi la Urusi.” Sababu ya pili ni kupinga simulizi la Urusi linalosisitiza usaidizi wa Urusi kwa nchi za Afrika katika mapambano yao dhidi ya ukoloni mamboleo na kwa maendeleo yao. Kulingana na Kyiv, Waafrika 3,000 hadi 4,000 wanapigana katika safu ya jeshi la Urusi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *