
ARUSHA: Mkuu wa Wilaya ya Arusha, Joseph Mkude, ameahidi kuchangia Bima ya Afya kwa Wote kwa waendesha bodaboda 60 kutoka vikundi 10, kila kikundi kikiwa na watu sita, ikiwa ni jitihada za kuwapatia uhakika wa huduma za matibabu wanapougua au kukumbwa na ajali zinazohusisha vyombo vya moto wanavyotumia.

Mkude ametoa ahadi hiyo leo wakati wa uzinduzi wa mpango wa ukopeshwaji pikipiki 22 kwa mikataba rafiki maarufu kama bodaboda kwa maofisa usafirishaji wa jiji hilo ambazo zimetoka kwa wadau wa maendeleo wakiwemo kampuni ya TVS ambao wametoa pikipiki 10 huku Umoja wa Bodaboda wa Arusha(UBOJA)Wilaya ya Arusha wakitoa pikipiki 12.

Amesema bima ya afya kwa wote ni muhimu ili kuepuka pale maofisa hao ambao hawana familia kupata matibabu pale yanapohitajika au wanapopata majanga wakiwa barabarani wakitoa huduma huku akisisitiza maofisa hao kuwa na nidhamu ya fedha na kurejesha kwa wakati marejesho ili wenzao wengine waweze kukopa na kujikwamua kiuchumi.

Naye Mwakilishi wa benki ya Azania, Pascal Sirili ameeleza nia ya dhati ya benki hiyo kuendelea kusapoti maofisa usafirishaji kwa kutoa mikopo yenye riba nafuu Kwa lengo la vijana kujikwamua kimaisha.