SHINYANGA: MKUU wa Mkoa wa Shinyanga, Mboni Mhita amesema maofisa maendeleo ya jamii na madiwani wasikwepe kusimamia mikopo ya asilimia 10 inayotolewa na halmashauri ili vikundi mbalimbali vyenye sifa vinufaike na mikopo hiyo.

Mboni Mhita amesema hayo kwenye mkutano wa hadhara alipokuwa akisikiliza kero mbalimbali katika mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye kijiji cha Segese Halmashauri ya  Msalala huku akieleza upo utaratibu wa kuunda vikundi na timu inayosimamia inajulikana.

Mhita amewataka madiwani na mkuu wa idara ya maendeleo ya jamii  kuwaeleza wananchi namna ya utolewaji wa mikopo hiyo na uandaaji wa vikundi kwani malalamiko mengi wananchi wamekuwa wakiyatoa ikiwemo wanapo hitaji kuandaa katiba ya vikundi inakuwa changamoto.

Mhita amesema wamekuwa wakitoa mikopo hiyo zaidi kwenye makundi ya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu ingawa wanaume nao wamekuwa wakihitaji wanachohofia badala ya kukuza uchumi wanaongeza mke wakati mwingine anapotea nyumbani tofauti na mwanamke anakuwa na watoto nakulisha familia.

“Mikopo ya asilimia 10 chanzo chake ni uwezeshaji wa fedha kutoka serikalini hivyo anawasihi wanawake wakope waachane na mikopo kausha damu mitaani yenye riba kubwa na kuwatesa hata kwenye familia zao,”amesema  Mhita.

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Msalala, Rose Manumba amesema utaratibu umekuwa ukifuatwa wa kuwapatia mafunzo kwanza na timu za kuwasimamia zinakuwepo na kuunda vikundi vya kuanzia watu watano na walemavu hata mmoja anaruhusiwa.

“Kuna zaidi ya  Sh milioni 557.7 zimetengwa katika awamu ya tatu ya utoaji wa mikopo kwa mwaka wa fefha 2025/2026 ambapo kundi la wanawake zimetengwa  zaidi ya Sh milioni 41.4,vijana zaidi ya Sh milioni 63.2 na watu wenye ulemavu zaidi ya Sh milioni 152.9,”amesema Manumba.

Mkazi wa kijiji cha Segese, Neema Emanuel katika mkutano huo amesema kero kubwa iliyopo watoto wamekuwa wamitaani sababu ya wanawake kujiingiza kwenye mikopo kausha damu nakutelekeza familia kwa kuogopa marejesho anakuwa hana aliomba kusiwepo urasimu katika kuunda vikundi na kupewa mikopo ya bila riba kwa haraka.

Mkazi wa kijiji cha Segese, Paul Alex amesema vijana wamekuwa tatizo aliomba wapatiwe mikopo ili waweze kufanya biashara nakutunza wazee wanapokosa inakuwa ni chanzo cha vurugu kwao

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *