WAZIRI wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dk Rhimo Nyansaho amezindua Bodi Mpya ya Ushauri ya Shirika la Uzalishaji Mali la Jeshi la Kujenga Taifa (SUMAJKT), Makao Makuu ya JKT Chamwino, jijini Dodoma, itakayoongozwa na Meja Jenerali Mstaafu Michael Isamuhyo, aliyemteua hivi karibuni.

Dk Nyansaho amempongeza Mwenyekiti na wajumbe wapya kwa kuteuliwa katika Bodi hiyo na kusema kuwa, SUMAJKT imepiga hatua kubwa na nzuri katika miaka ya hivi karibuni katika uzalishaji mali kwa kutekeleza miradi mingi yenye tija kwa Taifa na kuleta maendeleo.

Ametoa rai kwa bodi mpya aliyoizindua kushirikiana na menejimenti kuyaendeleza mafanikio hayo.

Amewataka pia kuongeza ubunifu ili uzalishaji na utendaji uimarike zaidi ndani ya shirika hilo kwa kuendeleza mambo mazuri yaliyoanzishwa na bodi iliyopita na kuweka mbele mikakati na ubunifu katika uwekezaji wa miradi mipya ili shirika lipige hatua kubwa zaidi katika kukidhi madhumuni ya kuanzishwa kwake mwaka 1981, pasipo kusahau suala la ulinzi na usalama.

Aidha, Dk Nyansaho amempongeza mwenyekiti aliyemaliza muda wake, Meja Jenerali Mstaafu Farah Mohamed na wajumbe wa Bodi, kwa kujituma, ubunifu na kazi nzuri iliyoleta mafanikio kwa shirika hilo.

Uzinduzi huo umehudhuriwa na Mwenyekiti aliyemaliza muda wake wa Bodi hiyo, Meja Jenerali mstaafu Farah Mohamed, Mwenyekiti Mpya wa Bodi Meja Jeneraki Michael Isamhyo na wajumbe wapya wa Bodi ya Ushauri, Mkuu wa JKT Meja Jenerali Rajabu Mabele, Mkurugenzi Mtendaji wa SUMAJKT, Brigedia Jenerali Petro Ngata, Mkuu wa Utawala JKT, Brigedia Jenerali Hassan Mabena na viongozi mbalimbali.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *