Halmashauri ya Jiji la Tanga imetangaza rasmi kwa wananchi kuanza kutuma maombi ya mikopo ya asilimia kumi inayotolewa na Halmashauri hiyo, kwa makundi ya Wanawake, Vijana pamoja na Watu Wenye Ulemavu.

Halmashauri ya Jiji la Tanga imetenga jumla ya shilingi bilioni mbili kwa ajili ya utoaji wa mikopo hiyo, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuwawezesha kiuchumi wananchi wa makundi maalum.

Akizungumza na waandishi wa habari, Mkuu wa Idara ya Maendeleo ya Jamii wa Halmashauri hiyo, Simon Mdende, amesema kuwa tangazo hilo litadumu kwa muda wa siku 31 kuanzia lilipotangazwa rasmi.

Amesema Halmashauri inawahimiza wanawake, vijana na watu wenye ulemavu kujitokeza kwa wingi kuwasilisha maombi yao ili kunufaika na fursa hiyo muhimu ya mikopo.

Simon Mdende ameongeza kuwa kwa sasa mikopo hiyo imeboreshwa zaidi ili kuhakikisha makundi husika yanapata mikopo kwa wakati, sambamba na kurahisisha taratibu za upatikanaji wake.

Hata hivyo, amewasisitiza wanufaika wa mikopo hiyo kuzingatia masharti ya marejesho ya mikopo kwa wakati, ili kutoa fursa kwa vikundi vingine vingi zaidi kunufaika.

Katika Halmashauri ya Jiji la Tanga jumla ya vikundi 452 tayari vimenufaika na mikopo ya asilimia kumi tangu kuanza kwa mpango huo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *