Kibaha, Pwani — Mkurugenzi Mtendaji wa taasisi isiyokuwa ya kiserikali ya Tanzania Women Empowerment Network (TAWEN), Dk. Florence Masunga, ametoa wito kwa wakuu wa taasisi za umma na viongozi wa taasisi mbalimbali nchini kujenga utamaduni wa kutenga bajeti maalum kwa ajili ya ukarabati wa miundombinu ili kuendelea kutoa huduma bora kwa jamii, hususan katika sekta ya afya.
Akizungumza leo Januari 16, 2026 katika mahafali ya 58 ya Chuo cha Afya na Sayansi Shirikishi cha Kibaha mkoani Pwani, Dk. Masunga amesema chuo hicho kilianzishwa mwaka 1968 na hadi sasa kimetimiza miaka 58, hali ambayo imesababisha baadhi ya miundombinu kuchakaa.
Amesema ukarabati wa mara kwa mara ni muhimu ili kuepuka gharama kubwa za kurejesha ubora wa majengo endapo yataachwa kwa muda mrefu bila matengenezo.
“Miaka 57 ni mingi, ni lazima miundombinu ichakae. Nawashauri viongozi wa taasisi kujenga utamaduni wa kukarabati kidogo kidogo kulingana na uwezo wa kifedha. Msisubiri hadi uharibifu uwe mkubwa,” amesema.
Akitumia methali ya Kiswahili “usipoziba ufa, utajenga ukuta,” Dk. Masunga amesisitiza umuhimu wa kuchukua hatua mapema, akiwashukuru pia wadau wanaoshirikiana na chuo hicho katika kuboresha mazingira ya kujifunzia.
Katika mahafali hayo, jumla ya wahitimu 108 walitunukiwa vyeti katika fani za utabibu, uuguzi na ukunga.
Mgeni rasmi amewataka wahitimu hao kujitunza, kutumia vyema taaluma zao kwa uadilifu na kuendelea kujiongezea elimu ili waweze kufikia ndoto zao na kuchangia maendeleo ya sekta ya afya nchini.
“Nimeona wahitimu wa miaka ya nyuma sasa wanashika nyadhifa mbalimbali katika utumishi wa umma na sekta binafsi. Nanyi fanyeni kazi kwa bidii mkilenga kulipa fadhila kwa Watanzania kwa kuwatumikia kwa uaminifu,” amesema.
#kilichoborakabi