SHINYANGA: MKUU wa Mkoa wa Shinyanga, Mboni Mhita ametoa zawadi ya Sh milioni 1.5 kwa walimu tisa na kombe la ushindi kwa wanafunzi wa Shule ya Msingi Nyabusalu kata ya Bulungwa Halmashauri ya Ushetu wilayani Kahama baada ya matokeo ya darasa la nne mwaka 2025 kuongoza kitaifa.
Mhita amekabidhi fedha na kombe jana baada ya kuitembelea shule hiyo ambapo alionana na walimu akiwa ameambatana na mbunge wa jimbo hilo Emmanuel Cherehan naye alikabidhi mashine ya kuchapisha shuleni hapo.

Mhita amesema kutokana na hali ilivyo si rahisi kuzania shule hii kushika nafasi ya kwanza kitaifa ukiangalia mazingira yake ni kijijini hasa lakini wazazi na walimu wamejitahidi kushikama kwa pamoja na kuwapa elimu inayostahili nakufikia hatua nzuri ya ufaulu.
“Nimeona kwenye taarifa yenu mnachangamoto ya ukosefu wa nyumba za walimu, vyumba vya madarasa, matundu ya vyoo ,mashine ya kuprinti, na ombi la kujengewa hosteli hivyo mkurugenzi na mbunge wote wako hapa na kilio chenu wamekisikia yatatekelezwa kazi mnayofanya wazazi kwa kushirikiana na walimu ni nzuri na shule zingine ziige mfano huu”amesema Mhita.
Mhita amesema juhudi iliyopo shule hii inatoa chakula kwa wanafunzi siku zote za shule mwaka mzima ila atahakikisha anafanya harambee ya wakulima wa zao la tumbaku wanaoishi kwenye halmashauri hii waweze kusaidia baadhi ya ujenzi wa miundombinu na walimu watajengewa nyumba moja yenye uwezo wa kuishi familia ya walimu sita ndani yake.
Mbunge wa jimbo la Ushetu Emmanuel Cherehani amesema baada ya kuona matokeo ya shule hiyo aliongea na mwalimu mkuu wa shule hiyo kuona mapungufu yaliyopo na maelekezo yoto yalikwisha tolewa na bajeti ya mwaka wa fedha 2026/2027 watajengewa nyumba za walimu na matundu ya vyoo.
“Shule hii imenifurahisha sana nimekabidhi zawadi ya mashine ya kuchapisha na jimbo hili kila mwaka huwa tunautaratibu wa walimu wote zaidi ya 1000 kukutana tumefanya miaka miwili mfululizo na walimu kueleza changamoto zilizopo kwenye shule zao baadhi zimekwisha tatuliwa”amesema Cherehani.
Ofisa Elimu Msingi wa Halmashauri hiyo Velena Ntulwa amesema kuna jumla wa shule za msingi 124 lakini kuna changamoto ya nyingi katika shule ya Nyabusalu iliyoshika nafasi ya kwanza kitaifa mafanikio ya ushindi wao ni ushirikiano mzuri wa wazazi na walimu na imekuwa ikitoa chakula wazazi kuchangia mwaka mzima bila kusimama.
Mwalimu Mkuu wa shule hiyo Mudamu Mbogo amesema shule hiyo inawanafunzi zaidi ya 500 darasa la kwanza hadi la saba ilianzishwa mwaka 1977 na imeweza kufanya vizuri kitaifa mara mbili mfululizo ila changamoto iliyopo walimu hawana nyumba za kuishi wengine wamepanga nyumba zisizo na hadhi,hakuna Mashine ya kuchapisha ,upungufu matundu ya vyoo na vyumba vya madarasa.
Baadhi ya wazazi wanaosomesha wanafunzi kwenye shule hiyo akiwemo Mudima Elias amesema ipo kamati ya shule ambayo walikubaliana kuchangia chakula kilo nane za maharage,ndoo ya ujazo wa lita kumi za mahindi na shilingi 8000 pia kila mwaka walikuwa wakitoa shilingi 4000 kwaajili ya kuchapisha mitihani.