Serikali imetangaza kutoa fursa kwa vijana zaidi ya 5,700 ya kujiunga na mafunzo ya uanagenzi yatakayowawezesha kupata ujuzi wa vitendo ili kushindana kikamilifu katika sekta za maendeleo kupitia ajira, kujiajiri na kuajiri wenzao.
Akitoa taarifa hiyo mapema leo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Ajira na Mahusiano, Deus Sangu amesema mafunzo hayo yanafadhiliwa na serikali kwa asilimia 100 huku yakihusisha fani mbalimbali za ufundi stadi zikiwemo ubunifu wa mitindo na ushonaji nguo, ufundi bomba, uashi, useremala, uchomeleaji na uungaji vyuma, upakaji rangi na maandishi ya alama, upishi, utengenezaji wa vipuri vya mitambo ambayo yatatolewa katika vyuo 47 nchini.
“Fani nyingine ambazo mafunzo halo yatatolewa ni umeme wa majumbani na viwandani, umeme wa magari, huduma za hoteli na utalii, ukataji madini na ufundi vyuma. Fani hizi ni muhimu sana kwa vijana wetu, kwa kuwa zitawawezesha kupata ujuzi ambao utawawezesha kuajiriwa au kujiajiri,” ameongeza Waziri Sangu
Mbali ya mafunzo hayo Waziri Deus Sangu amesema kuwa serikali inafanyia kazi afua mbalimbali za kujenga nguvu kazi yenye ujuzi wa kushinda katika soko la ajira za ndani na nje ya nchi.
“Afua zinazotekelezwa ni pamoja na Programu ya Taifa ya Kukuza Ujuzi kwa njia ya Uanagenzi”. Amesema Sanga
Katika hatua nyingine Waziri Sangu amevitaka vyuo vilivyopata dhamana ya kutoa mafunzo hayo kushirikiana na vijana waliochaguliwa, kuwafundisha na kuwasimamia vyema kipindi chote cha mafunzo yao huku akitoa wito kwa vijana waliochaguliwa kushiriki mafunzo kusoma kwa bidii, kuwa na nidhamu na kufuata sheria na taratibu za vyuo.
Mhariri @moseskwindi