Azarnykh mara kwa mara huchapisha picha zake akiwa na wapiganaji wapya, ikiwa ni pamoja na kundi la Wasyria ambao Omar alisafiri pamoja nao.

Chanzo cha picha, Telegram

Muda wa kusoma: Dakika 4

Miali ya moto inagusa kingo za pasipoti ya Omar.

“Inaungua vizuri,” anasema mwanamke asiyeonekana , akiongea kwa Kirusi, katika video hiyo.

Omar, mfanyakazi wa ujenzi raia wa Syria mwenye umri wa miaka 26, alikuwa tayari ametumwa kwa takribani miezi tisa kwenye mstari wa mbele wa vita vya Urusi nchini Ukraine wakati video hiyo ilipomfikia kwenye simu yake.

Aliitambua mara moja sauti ya mwanamke huyo. Ilikuwa ya Polina Alexandrovna Azarnykh, ambaye Omar anasema alimsaidia kujiunga na mapigano upande wa Urusi, akimuahidi kazi yenye mshahara mkubwa na uraia wa Urusi. Lakini sasa, mwanamke huyo alikuwa amekasirika.

Katika mfululizo wa ujumbe wa sauti uliorekodiwa nchini Ukraine, Omar, ambaye anatumia jina bandia kwa sababu za kiusalama, anaelezea jinsi alivyonaswa na kuishi kwa hofu kubwa ndani ya eneo la vita.

Anadai kuwa Azarnykh alimuahidi kwamba ikiwa atamlipa dola 3,000, atahakikisha hatatumwa kupigana vitani. Lakini kwa mujibu wa maelezo yake, alitumwa mstari wa mbele baada ya mafunzo ya siku 10 tu. Kwa sababu hiyo, alikataa kulipa pesa hizo, na hatimaye Azarnykh akaichoma pasipoti yake.

Anasema alijaribu kukataa kushiriki katika oparesheni moja, lakini wakubwa wake walimtishia kumuua au kumtia gerezani.

“Tulidanganywa… mwanamke huyu ni tapeli na muongo,” anasema Omar.

Azarnykh mara kwa mara huchapisha video zake akiwahamasisha watu kujiunga na kuhudumu katika jeshi la Urusi.

Chanzo cha picha, Telegram

Uchunguzi wa BBC Eye umefuatilia jinsi Azarnykh, mwalimu wa zamani mwenye umri wa miaka 40, anavyotumia kituo cha Telegram kuwavutia vijana wa kiume, hasa kutoka nchi masikini, kujiunga na jeshi la Urusi.

Ujumbe wa video wa mwalimu huyo wa zamani, akiwa anatabasamu, pamoja na machapisho yake yenye matumaini, yanatoa ofa za “mikataba ya mwaka mmoja” ya “kutumikia jeshi.”

Idhaa ya BBC World Service imeandika karibu kesi 500 ambapo iligundua kuwa alikuwa akitoa nyaraka zinazoitwa “mialiko”, ambazo humruhusu mpokeaji kuingia Urusi ili kujiunga na jeshi.

Mialiko hiyo ilitumwa kwa wanaume, hasa kutoka Syria, Misri na Yemen, ambao inaonekana walimpa taarifa zao za pasipoti ili kujiandikisha.

Hata hivyo, wapiganaji hao wapya na ndugu zao waliiambia BBC kwamba aliwadanganya wanaume hao waamini kuwa wangeepuka vita, hakuwafahamisha wazi kuwa hawangeweza kuondoka baada ya mwaka mmoja, na aliwatishia wale waliompinga. Alipowasiliana na BBC, alikanusha tuhuma hizo.

Familia kumi na mbili ziliiambia BBC kuhusu vijana waliodaiwa kuajiriwa kwa njia hiyo, ambao sasa wameripotiwa kufa au kutoweka.

Urusi hupoteza maelfu ya wanajeshi kila mwezi

Chanzo cha picha, ANDREY BORODULIN/AFP via Getty Images

Ndani ya nchi, Urusi imepanua uandikishaji wa lazima jeshini, imeajiri wafungwa, na imetoa bonasi kubwa zaidi za kujiunga na jeshi ili kuendeleza operesheni zake nchini Ukraine, licha ya kupoteza wanajeshi wengi.

Kwa mujibu wa NATO, zaidi ya wanajeshi milioni moja wa Urusi wameuawa au kujeruhiwa tangu kuanza kwa uvamizi mwaka 2022, wakiwemo wanajeshi 25,000 mwezi Desemba 2025 pekee.

Utafiti wa BBC News Russian, uliotegemea matangazo ya vifo na kumbukumbu nyingine za umma, unaonesha kuwa idadi ya wanajeshi wa Urusi waliouawa nchini Ukraine imeongezeka kwa kasi zaidi kuliko wakati wowote katika mwaka uliopita.

Ni vigumu kubaini idadi halisi ya wageni waliojiunga na jeshi la Urusi. Hata hivyo, uchambuzi wa BBC Russian, uliotazama pia idadi ya wageni waliouawa au kujeruhiwa, unaonesha kuwa takribani watu 20,000 wameandikishwa, wakiwemo raia wa nchi kama Cuba, Nepal na Korea Kaskazini.

Ukraine nayo imepata hasara kubwa miongoni mwa wanajeshi wake, na pia imewaingiza wapiganaji wa kigeni katika safu zake.

“Miili kila mahali”

Omar alikutana kwa mara ya kwanza Azarnykh mwezi Machi 2024, wakati alikuwa hana pesa kabisa kwenye uwanja wa ndege wa Moscow pamoja na Wasyria wengine 14.

Ajira nchini Syria zilikuwa chache na zenye malipo duni. Omar anasema kuwa meneja wa ajira alikuwa amewaahidi kazi waliyodhani ni ya raia ya kawaida ya kusimamia miundombinu ya mafuta nchini Urusi. Waliruka hadi Moscow, kisha kugundua kuwa walidanganywa.

Wakati wakitafuta njia mbadala mtandaoni, Omar anasema kuwa mmoja wa wanakundi hilo alimkuta Azarnykh kwenye jukwaa la Telegram na kumtumia ujumbe.

Alikutana nao uwanjani baada ya saa chache na kuwaongoza kwa treni hadi kituo cha kuajiri Bryansk, magharibi mwa Urusi, alisema.

Huko, anasema, aliwapa mikataba ya mwaka mmoja na jeshi la Urusi, yenye mshahara wa mwezi wa takribani dola 2,500 na bonasi ya kujiunga ya dola 5,000, kiasi ambacho kwao kilionekana kama ndoto tu nchini Syria.

Omar anaeleza kuwa mikataba hiyo iliandikwa kwa Kirusi, lugha ambayo hakuna aliyeifahamu, na kwamba alichukua pasipoti zao, akiahidi kuwa atawapata uraia wa Urusi. Pia aliwaahidi kuwa wataweza kuepuka kazi za kupigana ikiwa kila mmoja atamlipa dola 3,000 kutokakwenye bonasi yao, aliongeza.

Omar alielezea mapigano makali na milipuko ya mara kwa mara kwenye mstari wa mbele.

Chanzo cha picha, Roman Chop/Global Images Ukraine via Getty Images

Lakini, anasema, katika takribani mwezi mmoja, alijikuta kwenye mstari wa mbele akiwa na, kwa maelezo yake, mafunzo ya siku 10 tu na bila uzoefu wa kijeshi.

“Tutaaga dunia hapa asilimia 100,” alisema katika mojawapo ya ujumbe wake wa sauti, aliotuma kwa timu ya wachunguzi wa BBC.

“Wengi wamejeruhiwa, milipuko mingi, mabomu mengi. Usipokufa kwa mlipuko, utakufa chini ya mabaki yanayokupoteza,” alisema mwezi Mei 2024.

“Miili kila mahali… nimeiona kwa macho yangu, mtu anapokufa wanamweka kwenye begi la taka na kumuacha kando ya mti,” aliongeza.

Baada ya karibu mwaka mmoja, aligundua kile ambacho Azarnykh hakumweleza: amri ya Urusi ya mwaka 2022 inaruhusu jeshi kuendeleza mikataba ya wanajeshi moja kwa moja hadi mwisho wa vita.

“Ikiwa wataongeza mkataba, nimekwisha, Mungu wangu,” alisema.

Mkataba wake umeongezwa.

Mtandao wa Telegram wa Azarnykh una wanachama 21,000. Katika machapisho yake, mara kwa mara huwaalika wasomaji wanaotaka kujiunga na jeshi la Urusi kumtumia nakala iliyoskaniwa ya pasipoti yao.

Baadaye, huchapisha nyaraka za mialiko, mara nyingine zikihusishwa na orodha ya majina ya wanaume waliokuwa wametengwa.

BBC imeandika zaidi ya mialiko 490 kama hiyo ambayo ilitumwa katika mwaka uliopita kwa wanaume kutoka nchi kama Yemen, Syria, Misri, Moroko, Iraq, Côte d’Ivoire na Nigeria.

Machapisho yake yameelezea uajiri wa “kikosi cha kimataifa cha kipekee” na yanaweka wazi kwamba watu walioko Urusi bila mpangilio rasmi, ikiwa ni pamoja na wale ambao visa zao vimekwisha muda wake, wanaweza kuomba kujiunga.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *