
Nchini Uganda, matokeo ya kura ya uchaguzi mkuu uliofanyika siku ya Alhamisi, yanaendelea kutangazwa na tume ya Uchaguzi, wakati kiongozi wa upinzani Robert Kyagulanyi maarufu kama Bobi Wine, akizuiwa nyumbani kwa kuanzia Ijumaa asubuhi.
Imechapishwa:
Dakika 1 Wakati wa kusoma
Matangazo ya kibiashara
Hatua ya Bobi Wine kuzuiwa nyumbani kwake, kumekuja baada ya matokeo kuonesha kuwa mgombea wa chama tawala NRM rais Yoweri Museveni, anaongoza.
Kufikia mchana, kwa mujibu wa matokeo ya Tume ya uchaguzi Museveni mwenye umri wa miaka 81, ambaye amekuwa madarakani kwa miaka 40, alikuwa anaongoza kwa asilimia 76.2.
Mpinzani wake mkuu Bobi Wine mwenye umri wa miaka 43 naye, alikuwa na asilimia 19.85, wakati huu matokeo ya mwisho ya urais na ubunge, yakitarajiwa kutangazwa siku ya Jumamosi.
Hata kabla ya kuanza kutangazwa kwa matokeo, Bobi Wine alidai kuwa masanduku ya kupigia kura, yalikuwa yamejazwa kura bandia ili kumpa Museveni ushindi.
Uchaguzi nchini Uganda ulikumbwa na hitilafu baada ya mitambo ya kuwatambua wapiga kura kukwama, na vituo vingi vya kupigia kura nchini humo kufunguliwa kwa kuchelewa katika maeneo mengi ya nchi, huku mtandao wa Internet ukiwa umezimwa.