Bobi Wine

Chanzo cha picha, Getty Images

    • Author, Na Laillah Mohammed
  • Muda wa kusoma: Dakika 2

Polisi nchini Uganda wamekanusha madai kwamba mgombea kiti cha urais nchini humo kwa tiketi ya chama cha National Unity (NUP) Robert Ssentamu Kyagulanyi almaarufu Bobi Wine Pamoja na mke wake Barbara Kyagulanyi wamekamatwa, na kusisitiza kwamba wapo nyumbani kwao mjini Kampala.

Msemaji wa polisi nchini humo Kituuma Rusoke amesema kwamba maafisa wa usalama wameyazingira makazi yake Wine kwa sababu ya kisheria kwa kuwa yeye ni mgombea Urais na inawalazimu kuhakikisha usalama wake.

NUP: Wine alichukuliwa kwa nguvu nyumbani na helikopta

Kwa mujibu wa chama cha Bobi Wine, kiongozi huyo alikamatwa na vyombo vya usalama usiku wa Ijumaa Januari 16. Chama hicho kinadai kwamba helikopta ilitua katika eneo la nyumba yake jijini Kampala na kwamba “alichukuliwa kwa nguvu na kupelekwa kusikojulikana.”

Mwanawe mwanasiasa huyo Solomon Kampala pia amechapisha taarifa katika ukurasa wa X akisema kwamba hata mama yake Barbara Kyagulanyi amechukuliwa na polisi na kwa sasa wazazi wake wote hawako nyumbani.

Awali, mke wake Wine alinukuliwa akihojiwa na kituo cha redio kimoja nchini Uganda akizungumza kwa lunga ya Luganda kueleza taarifa kuhusu kukamatwa kwa mume wake na watu aliodai kuwa ni polisi.

Bobi Wine na wafuasi wake

Chanzo cha picha, Getty Images

Polisi: Madai ya Wine kukamatwa hayana msingi

Lakini polisi wanasisitiza kwamba madai hayo hayana msingi wowote na kwamba Wine yupo nyumbani kwake, mtaani Magere, wilayani Wakiso.

Mapema Jumamosi, Msemaji wa Polisi Kituuma Rusoke alipuuzilia mbali madai hayo na kuyataja kama taarifa za kughushi akisisitiza kwamba japo zimechapishwa na vyombo vya habari vya ndani na nje ya nchi, hakuna aliyethibitisha madai hayo kwamba Wine amekamatwa na wala ana zuiliwa na polisi wala jeshi la nchi.

Mtandao wa intaneti umeminywa

Kwa kuwa mtandao wa intaneti umeminywa kabisa nchini Uganda, imekuwa vigumu kuthibitisha madai hayo.

Hapo awali, Wine alisema kuwa amewekwa chini ya kizuizi cha nyumbani, huku vikosi vya usalama vikizingira makazi yake.

Katika hatua hiyo, msemaji wa polisi Kituuma Rusoke aliliambia shirika la utangazaji la ndani NBS kwamba kama mgombea urais, Wine alikuwa “mtu wa kuangaliwa”, na akaongeza kuwa uwepo mkubwa wa usalama kuzunguka nyumba yake ulikuwa kwa usalama wake mwenyewe.

Baadhi ya waandishi wa habari wa ndani walisema kuwa vikosi vya usalama vilikuwa vimewazuia kufika nyumbani kwa kiongozi huyo wa upinzani katika eneo la Magere, jijini Kampala.

Tume ya uchaguzi nchini Uganda inatarajiwa kutangaza matokeo rasmi ya kinyangayiro cha Urais leo Jumamosi.

Matokeo ya awali yanaonyesha kuwa Rais Yoweri Kaguta ameongoza kwa kishindo katika uchaguzi wa urais uliofanyika Alhamisi, akiwa mbali mbele ya mpinzani wake mkuu Bobi Wine, ambaye chama chake tayari kimeanza kuhoji uhalali wa matokeo.

Wine pia aliwaambia wafuasi wake wapuuze “matokeo ya uongo” yaliyotangazwa, akisema kuwa mamlaka “zinaiba kura”. Hakutoa ushahidi wowote kuhusu madai yake, na mamlaka husika hazijajibu tuhuma hizo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *