Serikali imewataka waajiri wote nchini kuzingatia amri ya kima cha chini cha mshahara kwa sekta binafsi, ambayo utekelezaji wake umeanza kutumika kuanzia Januari Mosi mwaka huu.
Ufafanuzi huo umetolewa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu- Kazi, Ajira na Mahusiano Deus Clement Sangu, ambapo amesema kwa mujibu wa amri iliyotangazwa Oktoba mwaka jana na waziri mwenye dhamana na masuala ya kazi, kima cha chini cha mshahara kimeongezeka kwa wastani wa asilimia 33.4 kutoka wastani wa Sh 275,060 kwa mwezi hadi Sh 358,322.
Sangu amesema ongezeko hilo ni la wastani wa jumla ikilinganishwa na kima cha chini kilichotangazwa mwaka 2022 ambacho kimefikia ukomo wake tarehe 31 Desemba mwaka jana.