Jeshi la Uganda limekanusha madai kwamba kiongozi wa upinzani Bobi Wine alitekwa akiwa nyumbani na kusafirishwa kusikojulikana kwa ndege ya kijeshi.

Imechapishwa: Imehaririwa:

Dakika 1 Wakati wa kusoma

Matangazo ya kibiashara

Taarifa ya jeshi imejiri wakati huu kura zikiendelea kuheshabiwa, karibia watu 10 wakiripotiwa kuuawa, mtandao wa intaneti ukiwa umezimwa.

Rais Yoweri Museveni, 81, anaelekea kutangazwa mshindi baadaye leo Jumamosi, matokeo yakionesha kuwa yuko mbele ya mpinzani wake Bobi Wine.

Mapema Ijumaa, Wine alikuwa ametangaza kwamba anazuiliwa nyumbani wake kabla ya chama chake baadaye kudai kuwa alichukuliwa kutoka nyumbani kwake kwa ndege ya kijeshi.

Tume ya uchaguzi nchini Uganda inatarajiwa kumtangaza Rais Museveni mshindi wa uchaguzi wa urais leo Jumamosi mchana
Tume ya uchaguzi nchini Uganda inatarajiwa kumtangaza Rais Museveni mshindi wa uchaguzi wa urais leo Jumamosi mchana REUTERS – Abubaker Lubowa

Jeshi limekanusha madai hayo yote kutoka kwa Wine na chama chake.

“Madai ya kukamatwa kwake hayana msingi wowote,” msemaji wa jeshi la Uganda Chris Magezi ameiambia AFP.

“Yanalenga kuwachochea wafuasi wake kuanza vurugu,” aliongeza.

Kulingana na AFP, kuna hali ya utulivu nje ya makazi ya Bobi Wine mapema leo Jumamosi japokuwa haikuweza kuwasiliana na chama cha Wine kutokana na changamoto za mawasiliano.

Rais wa Uganda Yoweri Museveni akiwa na mkewe Janet Museveni wakati wa kampeni nchini Uganda.
Rais wa Uganda Yoweri Museveni akiwa na mkewe Janet Museveni wakati wa kampeni nchini Uganda. REUTERS – Abubaker Lubowa

Majirani wa kiongozi huyo wa upinzani wameripoti kusikia sauti za ndege zisizo na rubani pamoja na helikopta usiku wa kuamkia leo, idadi kubwa ya maofisa wa usalama wakiwa kwenye eneo hilo.

Hadi kufikia jana Ijumaa, zaidi ya asilimia 80 ya kura zilikuwa zimehesabiwa, Museveni akiongoza kwa asilimia 73.7 dhidi ya 22.7 ya wine kwa mujibu wa matokeo ya tume ya uchaguzi ya Uganda.

Matokeo ya mwisho yanatarajiwa kutangazwa leo Jumamosi mchana.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *