
Rais wa Somalia Hassan Sheikh Mohamud amehudhuria sherehe ya kuapishwa kwa rais wa Jimbo la Kaskazini Mashariki huko Las Anod siku ya Jumamosi, Januari 17. Jamhuri ya Shirikisho ya Somalia inaundwa na majimbo yanayojitawala kwa sehemu. Jimbo la Kaskazini Mashariki ndilo lililoundwa hivi karibuni. Eneo hili, linalodaiwa na Somaliland, lilijiunga na Somalia mnamo mwezi Septemba 2025.
Imechapishwa:
Dakika 1 Wakati wa kusoma
Matangazo ya kibiashara
Na mwandishi wetu wa kikanda, Gaëlle Laleix
Ziara ya rais wa Somalia huko Las Anod ni ishara ya ushindi kuelekea eneo hili liliojitangaza taifa huru, ambalo lilijitenga na Somalia mnamo mwaka 1991 na limetambuliwa tu na Israel.
Kwa ziara hii, rais wa Somalia alitaka kutuma ujumbe ulio wazi: sio tu kwamba Somalia ni moja na haigawanyiki, lakini zaidi ya yote, ina washirika. Kwa sababu Hassan Sheikh Mohamud hakuja peke yake Las Anod, mji mkuu wa jimbo la kaskazini mashariki.
Siku ya Jumamosi, ujumbe mkubwa wa kidiplomasia uliandamana naye. Ndege moja kutoka Mogadishu iliwabeba mabalozi wa Sudan, Uturuki, na Saudi Arabia. Kulingana na SONNA, shirika la habari la Somalia, ujumbe kutoka Djibouti pia ulikutana na Rais Hassan Sheikh Mohamud huko Las Anod. Hii ilikuwa onyesho la mshikamano wa kikanda kwa umoja wa Somalia. Nchi hizi zote zililaani vikali tangazo la Israel kuitambua Somaliland mwishoni mwa mwezi Desemba.
Hargeisa haijatetereka na sherehe hiyo. Takriban kilomita 100 kutoka Las Anod, Somaliland ilifanya onyesho la nguvu Jumamosi, ikiandaa mazoezi ya kijeshi yaliyohusisha zaidi ya wanajeshi 6,000. “Somaliland ni taifa linalopenda amani, lakini amani haimaanishi kutofanya kazi,” aliandika Khadar Hussein Abdi, Waziri katika ofisi ya rais wa Somaliland, kwenye mtandao wa kijamii wa X. “Tuko tayari kuilinda nchi yetu na raia wetu.”