Mkuu wa Mkoa wa Songwe ndg Jabiri Makame amesema kuongezeka kwa ufanisi katika bandari ya DSM kumeongeza kiwango cha mzigo unaopita katika lango la Tunduma kwa mwaka, kutoka tani mil 5.4 mwaka 2022/23 hadi tani Mil 9.5 mwaka 2025 ambayo ni sawa na 75% ya Shehena unaosafirishwa kwenda nje ya Tanzania.
Hivyo, msongamano wa malori umeongezeka kwa kiwango kikubwa na kwamba, pamoja na miradi mingine ya kukabiliana na tatizo hili iliyopo, utekelezaji wa Mradi wa Bandari Kavu Tunduma utasaidia sana kuondoa msongamano kwa kiwango kikubwa na kurahisisha uvukaji wa Mpaka sambamba na kukuza biashara kati ya Tanzania na baadhi ya Nchi za SADC, kwani mradi huu pia unahusisha ujenzi wa barabara ya mchepuko kuelekea moja kwa moja katika eneo la kuvuka mpaka badala ya malori kupita katikati ya Mji wa Tunduma. Mradi huu pia ni sehemu ya ahadi ya Rais Mhe. Dkt Samia Suluhu Hassan wakati wa Kampeni zake Mkoani Songwe Mwaka 2025 na Utatekelezwa kwa Ubia kati ya Serikali na Sekta Binafsi.
RC Makame ameyasema hayo katika Kikao cha Wadau wa Utekelezaji wa Mradi kilichoitishwa na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Songwe na kuratibiwa na Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge na Wenye Ulemavu ndugu Dkt. Jim Yonazi ikiwa ni utekelezaji wa Maelekezo ya Waziri Mkuu Mhe. Dkt Mwigulu Nchemba aliyoyatoa katika Ziara yake Mkoani Songwe.
#kilichoborakabisa