Mwekezaji wa ndani, Leonard Bugomola Kiganga, amewekeza zaidi ya shilingi bilioni 2 katika mradi wa LENNY HOTELS LIMITED uliopo Bombambili, mkoani Geita, hatua inayotarajiwa kutoa ajira zisizopungua 200 kwa Watanzania. Mradi huo wa hoteli ulisajiliwa rasmi tarehe 6 Novemba 2024 na unaendelea kuwa mfano wa uwekezaji unaochochea uchumi wa ndani.

Leo, mradi huo umetembelewa na Mamlaka ya Kukuza na Kuwezesha Uwekezaji Tanzania (TISEZA) ikiwa ni sehemu ya ziara za kutambua na kuunga mkono miradi ya wawekezaji Watanzania. Ziara hiyo imelenga kuwafikishia wawekezaji fursa na vivutio mbalimbali vya kikodi vinavyotolewa na Serikali kwa wawekezaji wa ndani.

Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Mkuu wa Mkoa wa Geita ameikaribisha TISEZA mkoani humo na kusisitiza kuwa Serikali inaendelea kutoa kipaumbele kwa Watanzania kuwekeza, ikiwemo kutenga maeneo mahsusi ya uwekezaji mikoani pamoja na ardhi bure kwa ajili ya ujenzi wa viwanda na miradi mikubwa ya kimkakati.

Kwa upande wake, TISEZA imesisitiza kuwa neema ya vivutio vya uwekezaji inaendelea kuwafikia wawekezaji wa ndani, hususan katika sekta za huduma na uzalishaji, ili kuongeza thamani ya uchumi wa Taifa na kupanua wigo wa ajira.

Mradi wa LENNY HOTELS LIMITED unaonesha dhamira ya Serikali ya kuimarisha mazingira rafiki ya uwekezaji, huku wawekezaji wa ndani wakihimizwa kuchangamkia fursa zilizopo ili kuchochea maendeleo ya kijamii na kiuchumi Nchini.

#StarTvUpdate

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *