RAIS Samia Suluhu Hassan ametuma salamu za rambirambi kufuatia kifo cha Mzee Edwin Isaac Mbiliewi Mtei,, kilichotokea usiku wa Januari 19, 2026, jijini Arusha akisema amepokea taarifa hiyo kwa masikitiko makubwa.
Kwa mujibu wa taarifa ya Ikulu amesema alimkumbuka Marehemu Mtei kama mmoja wa watumishi na viongozi wenye mchango mkubwa katika ujenzi wa Taifa kwenye eneo la fedha, mipango na uchumi, aliyehudumu katika nafasi mbalimbali ikiwemo Gavana wa kwanza wa Benki Kuu ya Tanzania (1966 – 1974), na kushiriki kuimarisha misingi ya uendeshaji wa Benki Kuu na uthabiti wa mfumo wa fedha nchini.
“Kwa niaba ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kwa niaba yangu binafsi, natuma salamu za rambirambi kwa familia, ndugu, jamaa, marafiki, na wote walioguswa na msiba huu,” amesema Rais Samia.
Aidha, Rais Samia amesema Mzee Mtei ataenziwa katika historia ya siasa za vyama vingi kama miongoni mwa waasisi wa demokrasia ya ushindani wa vyama, akitajwa kuwa ni miongoni mwa waanzilishi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA).
Ameongeza kuwa, mchango wa Marehemu utaendelea kukumbukwa na kuenziwa na vizazi vya sasa na vijavyo, hususan kupitia maandiko yake binafsi (autobigraphy) yanayoeleza safari yake ya maisha na utumishi wake wa uongozi katika kuijenga Tanzania.
“Rais Samia anawaombea faraja, nguvu na amani; familia, ndugu na wafiwa wote, na kumuomba Mwenyezi Mungu ailaze roho ya Marehemu mahali pema peponi, Amina.” imesema taarifa hiyo.
