Nigeria inakabiliwa na changamoto nyingi za kiusalama

Chanzo cha picha, Getty Images

Makundi yenye silaha yamewateka nyara makumi ya watu waliokuwa wakihudhuria ibada katika makanisa mawili katika jimbo la Kaduna, Nigeria, kwa mujibu wa polisi wa eneo hilo.

Kiongozi mmoja mwandamizi wa kanisa alisema waumini zaidi ya 160 walitekwa nyara na watu wenye silaha wakati wa ibada ya Jumapili.

Hili ni tukio la hivi karibuni katika wimbi la utekaji nyara wa halaiki nchini Nigeria, ambapo Wakristo na Waislamu wote wamekuwa wakilengwa.

Makundi hayo, yanayojulikana kijijini kama “bandits”, mara kwa mara hufanya mashambulizi kama hayo katika maeneo ya kaskazini na kati mwa nchi ili kupata fedha za fidia.

Akielezea shambulio la Jumapili, polisi wa eneo hilo walisema watu waliokuwa na “silaha za kisasa” waliingia kwa nguvu katika makanisa hayo mawili yaliyopo Kurmin Wali, jamii ya msituni katika kata ya Afogo, mnamo saa 11:25 kwa saa za huko.

“Washambuliaji walikuja kwa idadi kubwa, wakaziba njia za kuingia makanisani na kuwalazimisha waumini kutoka na kuingia porini,” alisema Mchungaji Joseph Hayab, mkuu wa Shirika la Kikristo la Nigeria (CAN) kwa kanda ya kaskazini, alipoliambia shirika la habari la AFP siku ya Jumatatu.

Akizungumza na Reuters, Hayab aliongeza: “Taarifa nilizopokea kutoka kwa wazee wa makanisa zinaeleza kuwa waumini 172 walitekwa nyara, huku tisa wakifanikiwa kutoroka.”

Mwezi Novemba, wanafunzi na walimu zaidi ya 300 walitekwa nyara kutoka shule moja ya Kikatoliki. Baadaye waliachiliwa kwa makundi mawili tofauti. Tukio hilo lilikuwa miongoni mwa msururu wa matukio ya utekaji nyara yaliyopewa uzito mkubwa na vyombo vya habari vya kimataifa.

Nigeria inakabiliwa na changamoto nyingi za kiusalama, zikiwemo utekaji nyara wa kuomba fidia unaofanywa na magenge ya kihalifu, uasi wa wanamgambo wa Kiislamu kaskazini-mashariki, ghasia za kujitenga kusini-mashariki, pamoja na mapambano kati ya wafugaji na wakulima katika eneo la kati juu ya upatikanaji wa ardhi na maji.

Unaweza kusoma;

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *