Waziri Mkuu wa Hispania, Pedro Sánchez, ameahidi kufuatilia kwa kina sababu za treni mbili za mwendo kasi kugongana kusini mwa Hispania, ajali iliyosababisha vifo vya takribani watu 40, huku waokoaji wakiendelea kuchunguza mabaki ya treni hizo.

Baada ya kutembelea eneo la ajali, Sánchez pia alitangaza siku tatu za maombolezo ya kitaifa kwa heshima ya waathiriwa.

Zaidi ya watu 120 wengine walijeruhiwa baada ya mabehewa ya treni iliyokuwa ikielekea Madrid kuacha reli na kuvuka hadi njia ya reli ya upande wa pili, kisha kugongana na treni nyingine iliyokuwa ikisafiri kuelekea Adamuz, Jumapili jioni.

Ajali hiyo ni mbaya zaidi kuwahi kutokea nchini humo katika kipindi cha zaidi ya muongo mmoja.

Mwendeshaji wa mtandao wa reli, Adif, alisema kuwa ajali hiyo ilitokea saa 19:45 kwa saa za huko (18:45 GMT) siku ya Jumapili, takribani saa moja baada ya moja ya treni kuondoka Málaga kuelekea kaskazini hadi Madrid, ilipoacha reli katika sehemu ya reli iliyonyooka karibu na mji wa Córdoba.

Kwa mujibu wa Waziri wa Uchukuzi, Óscar Puente, nguvu ya mgongano ilisukuma mabehewa ya treni ya pili hadi kwenye tuta la udongo. Aliongeza kuwa wengi wa waliopoteza maisha na kujeruhiwa walikuwa katika mabehewa ya mbele ya treni ya pili, ambayo ilikuwa ikisafiri kusini kutoka Madrid kuelekea Huelva.

Timu za uokoaji zilisema mabaki ya treni yaliyopinda na kuharibika vibaya yalifanya iwe vigumu kuwaokoa watu waliokuwa wamenaswa ndani ya mabehewa.

Sánchez alitembelea eneo la ajali hiyo pamoja na maafisa wakuu wa serikali siku ya Jumatatu alasiri.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *