Naibu Waziri wa Fedha, Laurent Luswetula, ameitaka Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kuimarisha udhibiti wa sekta ya fedha nchini ili kuwalinda wananchi dhidi ya vitendo vya ulaghai na mikopo kandamizi maarufu kama kausha damu inayotolewa na taasisi zisizo rasmi. Amesema mikopo hiyo imekuwa chanzo cha wananchi wengi kupoteza mali na vitu vyao vya thamani.
Luswetula amesema ni muhimu kwa BoT kuhakikisha kuwa taasisi zote za kifedha zinafanya kazi kwa kuzingatia sheria na taratibu zilizopo, hatua itakayosaidia kujenga mfumo salama na endelevu wa kifedha kwa wananchi.
Naibu Waziri ameyasema hayo jijini Tanga wakati wa maadhimisho ya Wiki ya Huduma za Kifedha Kitaifa, yanayoshirikisha taasisi mbalimbali za kifedha nchini. Maadhimisho hayo yalianza rasmi Januari 19 na yanatarajiwa kufikia kilele chake Januari 26, 2026, yakibeba kaulimbiu isemayo, “Elimu ya Fedha, Msingi wa Maendeleo ya Kiuchumi na Jamii.”
Aidha, amezitaka taasisi za fedha nchini kuhakikisha zinawashirikisha wananchi kwa kuwapatia elimu ya fedha, hususan juu ya matumizi sahihi ya mikopo, ili waweze kujikwamua kiuchumi na kuepukana na mikopo kandamizi.
#StarTvUpdate

(Feed generated with FetchRSS)